MKUU wa Mkoa wa K i l i m a n j a r o , Leonidas Gama ameagiza sukari i l i y o k a m a t w a
wilayani Rombo ikiwa inapelekwa nchini Kenya kuuzwa kwa wananchi kwa Sh 1,900.

Gama alimpa agizo hilo Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Peter Toima baada ya sukari hiyo kukamatwa kutokana na agizo la Serikali la kupiga marufuku uuzaji wa sukari nje ya nchi.

Sukari wilayani hapa kwa sasa inauzwa kati ya Sh 2,500 na Sh 2,700 kutokana na bidhaa hiyo
kuadimika nchini.

Pamoja na agizo la serikali kuzuia sukari kuuzwa nje ya nchi hali hiyo iliendelea hadi pale
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipoishutumu Polisi kuwa inashirikiana na wahujumu uchumi
kusafirisha sukari nje ya nchi.

Baada ya tuhuma hizo za Pinda, polisi walizinduka na kuanza kukamata shehena nyingi zilizokuwa zinapelekwa nchini Kenya.

Agizo hilo la RC lilipongezwa na wananchi wilayani hapa kwa maelezo kuwa mbali na magendo
ya sukari, lakini wamekuwa wakikumbwa na njaa kila mara kutokana na ukame na wanyama
waharibifu, huku wafanyabiashara wasio waaminifu wakipitisha nafaka na kwenda kuiuza Kenya.

Walisema wafanyabiashara hao wanapeleka Kenya nafaka kama mchele, mahindi na sukari ambako wanapata faida nyingi na kuwaacha wananchi wakiteseka na njaa.



Gama aliwaahidi wananchi hao kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama katika wilaya
hiyo kukomesha kabisa tabia hiyo ya usafirishaji nafaka nje ya nchi, kwani mbali na kukiuka kanuni na taratibu, pia wanaharibu miundombinu hasa barabara ambayo bado ujenzi wake haujakamilika.

Wakati huo huo, mkuu huyo wa mkoa amewataka wafanyakazi katika halmashauri zote nchini, kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na nidhamu, ili wawaletee wananchi maendeleo.

Gama aliyepo katika ziara yake ya siku mbili wilayani humo, kukagua shughuli za maendeleo, alisema hayo alipokuwa akizungumza na watendaji wa halmashauri hiyo.

Alisema ili kuleta maendeleo ni vema wafanyakazi wawepo kazini kwa muda wote wa kazi badala ya kuripoti kazini na kuondoka kama wafanyavyo wafanyakazi wengi siku hizi.

“Suala la kuondoa umasikini lipo mikononi mwetu, kama Watanzania wote watafanya kazi kwa ari, nchi hii itakuwa ya kihistoria kwa kiwango kikubwa cha maendeleo tutakachokipata,” alisema Gama.

Alisema ni lazima halmashauri zote ziwe na mikakati ya wazi ya kuondoa umasikini kwa wananchi wake kwa kutumia wataalamu.

Gama alionya kuwa rushwa na magendo ni kiini cha ukosefu wa uadilifu na uaminifu na kuwataka watumishi hao kutekeleza wajibu wao kwa moyo wote na kuacha kufanya siasa maofisini.

Awali Gama aliwataka watumishi hao kutunza siri za Serikali hasa katika mazingira hayo ya
mfumo wa vyama vingi kwa kuzingatia kanuni na maadili ya kazi zao.