Wodi za Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) jijini Dar es Salaam zimeendelea kukabiliwa na msongamano kutokana na wgonjwa kukosa vitanda na kujikuta wakiwa wamelala chini katika veranda.
Wodi 17 na 18 katika jengo la Sewahaji bado zimefurika wagonjwa wa ajali za barabarani.
NIPASHE imetembelea wodi hizo na kukuta wagonjwa hao wakiwa katika mazingira yasiyoridhisha kutokana na waliolala chini kutowekewa vyandarua na wengine walirukiwa na nzi.
Mmoja wa wauguzi alisema kuwa kuna ukosefu wa vyandarua pamoja na sehemu ambayo wanalalia katika veranda imekuwa vigumu kufunga vyandarua.
“Kama unavyoona huku kwenye veranda wagonjwa walivyojazana hata kufunga neti inashindikana kwa kuwa eneo hilo linatumika kwa ajili ya watu kupita,” alisema kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Alisema ajali zimekuwa zikiongezeka hali ambayo inasababishia wodi hizo kufurika wagonjwa na kujikuta wengine kulazimika kuwekewa magodoro katika veranda.

NIPASHE ilivyotembelea wodi hizo iliwakuta wagonjwa hao wakiwa wamelala huku wengine wakipandwa na nzi.
Afisa Uhusiano wa Moi, Jumaa Almasi, alisema hali ya msongamano inaendelea kuzikabili wodi hizo kutokana na ongezeko la ajali.
Alisema kuwa kuna wakati mwingine idadi inapungua kwa kiwango na badaye kuongezeka, hivyo kuwa vigumu msongamano kupungua.
Alisema ajali zimeongezeka, lakini pikipiki ni nyingi zaidi kwa kuwa kila siku wanapokea majeruhi watano hadi kumi.
Almasi alisema wodi moja ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 35, lakini kwa siku hospitali hiyo inapokea majeruhi 30 hadi 40 wa ajali tofauti.
Hata hivyo, alisema kwa sasa wamejipanga kukabiliana na tatizo hilo kwa kutumia teknolojia mpya ya kisasa ya Sign Knaic ambayo mtu akifika ambaye amepata ajali anatibiwa kwa siku tatu na kuruhusiwa.
Alisema pia Moi ina utaratibu wa kubadilishana uzoefu na wataalamu wengine katika kutibu magonjwa ya mifupa ili wawe wanatoa tiba katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha hospitali hiyo inapokea wagonjwa ambao kesi zao ni kubwa.
Aidha, alisema kwa sasa wapo katika mchakato wa maandalizi ya kupanua taasisi hiyo kuanzia Februari, 2011.
CHANZO: NIPASHE