Wapiganaji wa kabila la Tuareg waliorudi Mali kutoka Libya wanaaminika kusaidia katika kuanzisha kundi jipya la waasi.
Kundi hilo la National Movement for the Liberation la Azawad NMLA limesema ni matokeo ya muungano baina ya makundi mawili ya waasi, yaliyoongezwa nguvu na Watuareg waliopigana kwa ajili ya Kanali Muammar Gaddafi nchini Libya.

Watuareg wa Mali wamelalamika kwa muda mrefu kwa kutengwa na serikali ya kusini.

NMLA wanataka uhuru wa eneo la jangwa kaskazini mwa Mali.

Watuareg ni jamii ya kuhamahama ambao aghlabu huishi katika jangwa la Sahara na karibu na miji kwenye nchi kaskazini na magharibi mwa Afrika.

Tangu mwanzo wa mgogoro wa Libya Mali imekuwa ikisema kuanguka kwa Kanali Gaddafi kutaathiri utulivu eneo hilo.

Mwandishi wa BBC Martin Vog kwenye mji mkuu, Bamako, amesema jambo linalotokea sasa ni sababu ya Mali kuunga mkono nafasi ya Libya kwenye Umoja wa Afrika, ambayo ilipendelea kutatua tatizo lililopo kwa mazungumzo badala ya kampeni ya kurusha mabomu inayofanywa na Nato.

Mwandishi wetu alisema Watuareg wenye ndoto za kuwa na uasi mpya wameamua kutumia wakati huu, kwa kurejesha kaka zao wenye silaha madhubuti na wenye mafunzo thabiti, kuonyesha msimamo wao halisi.

Alisema matakwa yao ni yenye uzito zaidi kuliko makundi ya waasi wa awali.