TAMBO, matumaini, hofu zimetanda miongoni mwa wapenzi na mashabiki wa timu kubwa mbili, Yanga na Simba zinazokwaana keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya Ligi Kuu.

Juzi na jana, minong'ono zaidi ilikuwa kwa wapenzi wa Yanga kuzungumzia hatua ya uongozi kubadili benchi la ufundi katikati ya ligi na pia kuelekea katika mechi ngumu ya mahasimu.

Yanga ambayo ndiyo mwenyeji wa mchezo huo, ilimwondoa Sam Timbe katika benchi la ufundi na nafasi yake kuchukuliwa na Kosta Papic, ambaye ataliongoza jahazi la Yanga hadi mwisho wa msimu.

Mwananchi ilifanya mahojiano na wadau mbalimbali juu ya mpambano huo, na mmoja wao ni mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Kitwana Manara aliyesema kwa uzoefu wake, mechi ya Simba na Yanga inaweza kuongozwa na mtu yoyote hata kama hana taaluma ya ukocha.

Manara ambaye alitamba zaidi katika medani ya soka kwenye miaka ya 60 na 80 alisema kutokana na hali hiyo hatashangwazwa kuona timu ya Yanga ikifanya vizuri katika mchezo wake wa Jumamosi dhidi ya Simba japokuwa imelifanyia mabadiliko benchi lake la ufundi wakati ikiwa na mchezo mugum mbele yake.



Wakati Manara akisema hayo, baadhi ya wapenzi na mashabiki wa Yanga katika vijiwe mbalimbali, wanaonekana kujawa na hofu kwa timu yao kufanya vibaya kwa kile walichodai kuwa Simba wapo vizuri na wameonyesha kiwango cha hali ya juu.

Katika kutia chachu, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi 'kuisapoti' timu yao iondoke na ushindi dhidi ya Yanga huku beki wake, Victor Costa akiwatoa wasiwasi.

Rage aliiambia Mwanachi jana kuwa ana imani na kikosi na kuahidi kuweka heshima ya kutofungwa hadi kumalizika mzunguko wa kwanza.

Wakati Rage akisema hayo, wajumbe wa kamati ndogondogo za timu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, jana jioni walipeleka baraka kwa wachezaji wao waliopiga kambi Bamba Beach Kigamboni kujiandaa kwa mchezo huo.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu' alisema kuwa kamati zinakwenda kuzungumza na wachezaji kuwapa mawili, matatu kuelekea kwenye mchezo huo.

Naye kocha wa Simba, Moses Basena alisema kuwa anatamani mchezo huo uwe kesho kwa jinsi alivyojiandaa vizuri na kikosi chake kipo kamili kwa mchezo huo.

"Kulikuwa na tatizo kidogo upande wa mabeki lakini nimelimaliza na Victor Costa amerudi baada ya kuwa mgonjwa kwa hiyo sina wasi wasi," alisema Basena.

Alisema ingawa lolote linaweza kutokea katika mpira kwa kuwa hautabiriki lakini uhakika wa kushinda ni mkubwa.

Mbali na Simba, uongozi wa Yanga umeimarisha ulinzi mara dufu kwenye kambi ya timu hiyo kabla ya mpambano huo wa keshokutwa kwa kile kilichoelezwa kuhofia kuhujumiwa.

Ofisa habari wa Yanga, Luis Sendeu alisema kuna tetesi za hujuma kupenyezwa kwa wachezaji ili timu ifanye vibaya keshokutwa. Yanga inaingia kambini leo kwenye Hoteli ya Courtyard Protea iliyopo Upanga, Dar es Salaam.

Alisema kutokana na hali hiyo, wamepiga marufuku baadhi ya makundi ya watu kuhudhuria mazoezi yanayoendelea Shule ya Kimataifa ya Tanganyika, IST, Masaki ikiwa ni pamoja na kusogelea kambi ya timu hiyo ambayo awali ilikuwa Makao Makuu ya klabu hiyo Mitaa wa Twiga na Jangwani.

"Hali hii ya hujuma inatutisha sana, ndio maana tumeamua tuimarishe ulinzi wa timu na tuipeleke sehemu nyingine na yeyote atakayethubu kupenyeza mbinu chafu tukimbaini atachukuliwa hatua kali.

Yanga itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kunyukwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii na katika mzunguko wa pili msimu uliopita iliyochezwa Machi 5 mwaka huu timu hizo zilitoka sare ya 1-1 na kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi Simba waliwanyuka Yanga mabao 2-0.

Katika hatua nyingine, tiketi za mpambano huo wa watani, zitaanza kuuzwa kesho katika maeneo mbalimbali jijini kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah.

Imeandaliwa na Vicky Kimaro, Sweetbert Lukonge, Kalunde Jamal na Jesca Nangawe.