Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini(IGP) Said Mwema(kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,kuhusu matukio ya vikundi vya kigaidi yanayoendelea katika nchi za Afrika mashariki.

JESHI la Polisi limetoa hadhari kuhusu uwezekano wa kutokea kwa vitendo vya ugaidi hivyo kutaka wananchi kuchukua tahadhari hasa kwa wageni wanaoingia nchini ambao wanaweza kutumiwa na vikundi vya ugaidi duniani kuhujumu nchi.

Tahadhari hiyo ya polisi inakuja kipindi ambacho tayari nchi jirani ya Kenya, imeshambulia na watu wanaodhaniwa ni kutoka kundi la kigaidi la Al – shabaab, lenye makazi yake nchini Somalia. Jana, katika kujihadhari na uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi nchini, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP),Said Mwema aliitisha mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuzungumzia kitisho hicho.

IGP Mwema alisema mara nyingi magaidi hao wamekuwa wakiwarubuni wananchi ili washiriki vitendo hivyo, jambo ambalo liliwahi kusababisha maafa mwaka 1998 baada ya magaidi wanaotuhumiwa kuwa na mtandao wa Alqaeda kulipua ubalozi wa Marekani nchini. Mkuu huyo wa jeshi la polisi alisema kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kuwa makini na wageni ambao wanaweza kuwahisi kuwa na mafungamano na magaidi hao.



Alisema magaidi wanaweza kutumia ukaribu wao na wananchi ili kutimiza malengo waliyokusudia, jambo ambalo linaweza kuathiri shughuli za maendeleo.
“Nchi jirani kuna vitendo vya ugaidi vinavyojitokeza ambavyo vimeweza kuhatarisha amani ya nchi, kutokana na hali hiyo wananchi wanapaswa kuwa makini na wageni wanaoingia au kutoka ambao wanaweza kuwatilia shaka ili waweze kukaguliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,”alisema IGP Mwema.
IGP Mwema alisema wananchi wanapaswa kuwa makini na wageni wote wanaoingia na kutoka nchini, ambao baadhi wanaweza kutumiwa na kundi la Al-shabaab kufanya matukio kama ya Kenya, ambayo yanahatarisha amani ya nchi.

Alisema kundi hilo lina mtandao mkubwa ndani na nje ya Afrika na kwamba linafadhiliwa na kundi kubwa la kigaidi duniani la Alqaeda. Kwa mujibu wa mkuu huyo wa jeshi la Polisi uhalifu wa genge hilo ni wa kimataifa hivyo basi wanahitaji juhudi za ziada ili kupambana nao. Alisema kutokana na hali hiyo wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwa wataona dalili ya kuwepo kwa watu wa aina hiyo ili waweze kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mwema alisema jeshi la polisi linashirikiana na wadau mbalimbali wa ulinzi na usalama, ili kuhakikisha kuwa hali ya nchi inaendelea kuwa tulivu na kwamba hakuna kikundi chochote kitakachoweza kufanya mashambulizi kama hayo.

Hivi karibuni ukanda wa Afrika Mashariki umekumbwa na kitisho cha matukio ya kigaidi baada ya kundi la Alshabaab kucharuka na kufanya vitendo vya utekaji nyara wageni nchini Kenya huku pia wakikosa kuteka meli katika ukanda wa habari ya Tanzania. Kutokana na utekaji nyara huo, Kenya iliamua kupeleka jeshi nchini Somalia kupambana na kundi hilo.