WAZIRI wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Gaudentia Kabaka jana alifanya ziara ya ghafla katika Hoteli ya Holiday Inn ya jijini Dar es Salaam na kugundua ukiukwaji wa sheria za kazi.
Waziri Kabaka alichukua uamuzi huo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hiyo.
Waziri Kabaka alithibitisha kuwa hoteli hiyo haikuwa na tawi la Chama Wafanyakazi wa Hifadhi za Taifa, Mahoteli na Majumbani (CHODAWU).
Baada ya kujionea kasoro hizo, Waziri Kabaka aliagiza hoteli hiyo ipelekewe hati ya Amri Tekelezi inayoagiza menejimenti kutekelezwa matakwa ya sheria za kazi.
Waziri Kabaka alisema baada ya kupewa hati hiyo watakaguliwa mara tatu na wakikutwa hawajatekeleza matakwa hayo ya sheria watapelekwa mahakamani.
Alimuagiza Ofisa Kazi wa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana anayeshughulikia wilaya za Ilala na Kinondoni, Nestory Mloka kufanya ukaguzi wiki ijayo na kuwapatia hati hiyo ili waanze utekelezaji wa matakwa ya sheria hiyo ikiwemo kuwa na mkataba wa hali bora sehemu za kazi.
Akizungumza katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hoteli hiyo, Ronnie Pieters, viongozi wa Chodawu Mkoa na Wilaya, Waziri Kabaka aliagiza wawekezaji wanaofanya kazi katika ofisi hiyo wapeleke ofisini kwake nakala za hati zilizowaruhusu kufanya kazi nchini.
Ofisa Rasilimaliwatu wa Hoteli hiyo, Gasper Simbachawene alimueleza waziri kuwa hoteli hiyo ina wafanyakazi 146 wanaolipwa mishahara ya kima cha chini Sh 180,000 hadi Sh 200,000, jambo lililopingwa na baadhi ya wafanyakazi hotelini hapo.
0 Comments