MIILI ya watu 12 walioteketea kwa moto katika ajali ya basi la Deluxe Coach iliyotokea Misugusugu mkoani Pwani juzi, watazikwa leo na Serikali kwa heshima zote katika kaburi moja katika eneo la Air Msae mjini Kibaha.

Eneo hilo ndipo walipozikwa watu waliopata ajali ya basi la Air Msae lililokuwa likitokea Arusha kuja Dar es Salaam miaka ya 1990.

Uamuzi huo umefikiwa jana katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani, iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mwantumu Mahiza kutokana na miili hiyo kuharibika vibaya na kushindwa kutambulika.

Akizungumzia mazishi hayo jana, Mahiza alisema kabla ya maziko, miili ya watu hao itachukuliwa sampuli kwa ajili ya vipimo vya vinasaba (DNA) ili vifanikishe utambuzi wao.

Taarifa kutoka Hosptali Teule ya Tumbi, zilieleza kuwa hata wananchi waliokwenda kujaribu kutambua ndugu zao, walishindwa kufanya hivyo kutokana na kuharibika kwa miili hiyo ambayo baadhi imekuwa majivu.

Kutokana na hali hiyo, Mahiza aliwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kufanikisha kuwatambua ndugu zao, kwa kupeleka vitu kama nguo ambazo ndugu zao walizitumia siku chache kabla ya ajali hiyo.



"Tunaomba wananchi walioondokewa na ndugu zao katika ajali hii watoe ushirikino kwa kuleta vitu kama soksi, shati, khanga au viatu alivyokuwa anatumia ndugu yao hivi karibuni ambavyo havijafuliwa ili visaidie kutambuliwa baada ya kupimwa kwa njia ya vinasaba,” alisema Mahiza.

Ofisa Habari wa Hosptali Teule ya Tumbi, Rose Mtei alisema kuwa majeruhi waliofikishwa katika hospitali hiyo ni 36 ambapo 35 waliruhusiwa na mmoja aliyelazwa anaendelea vizuri.

"Kutokana na ajali hiyo ndugu wamefika kujaribu kutambua miili hiyo lakini haikuwezekana kutokana na kuharibika vibaya na wengi wamekuwa majivu, kwa sasa tunasubiri tamko la uongozi wa Mkoa ili kujua mazishi yatakuwa wapi,” alisema Mtei kabla ya tamko la Mahiza.

Kati ya miili hiyo 12, ni miili mitano tu ambayo inaonekana kama miili ya watu lakini haitambuliki ya nani na miili mingine imekuwa majivu kabisa.

Mtei aliwataja baadhi ya majeruhi waliofikishwa katika hospitali hiyo ni Julias Lesiwa, Mary Mbunga, Earnest Kato, Charles Nyaongo, Shukuru Jarious, Daniel Michael, Nestory Mfuse, Benedictory Labure na Jumanne Mjif.

Wengine ni Omary Omary, Fred Sarom, Paschal Amos, Neema Mgomba, Augustine Matei, Omary Jahu, Maburuk Mohamed Cecilia Ngirao, Alfred Semwari, Isack Manyota, Kelvin Ndugu, Jamira Sefu, Veronica Hippill, Tobias Legume, Mashaka Muganyizi, Paschal Lungwa na Amina Michael.

Ajali hiyo ilitokea baada ya basi hilo namba T 334 AAD aina ya Volvo lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, kupasuka tairi la mbele kulia na kupinduka na kushika moto.

Akizungumzia ajali hiyo jana Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga alisema tayari Jeshi la Polisi limepeleka wataalamu wake wa vinasaba kuchunguza majivu na mabaki ya watu waliokufa katika ajali hiyo.

“Kuna wataalamu wetu wamekwenda Kibaha kuchukua majivu ili kupima vinasaba na kubaini ni watu wangapi waliopoteza maisha katika tukio hilo,” alisema.

Alisema mpaka sasa mbali miili hiyo kushindwa kutambuliwa, watu wanane bado hawajatambuliwa wala haijulikani waliko.

Kamanda Mpinga alisema basi hilo liliondoka Dar es Salaam likiwa na abiria 49 na kuwataka madereva kuwa makini wawapo barabarani kwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, ili kuepusha matukio ya ajali.

Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amemtumia Mkuu wa Mkoa wa Pwani salamu za rambirambi na masikitiko makubwa kwa ajali hiyo.

“Hii ni ajali mbaya sana, ni ajali ya kusikitisha sana na ya kuhuzunisha kwa wananchi wote na hasa mimi,” Rais alisema na kusisitiza kuwa ajali kama hizi zinazidi kutoa changamoto kwa Polisi na vyombo vya usalama barabarani.

“Huu ni mtihani zaidi kwa Polisi na vyombo vya usalama barabarani, tunahimiza sheria za barabarani zifuatwe na kuzingatiwa, na hili ni pamoja na usalama wa vyombo hivyo na abiria wao, hii ni changamoto kubwa kwa Polisi katika kulisimamia hili na kuona linatekelezwa,” alisema katika taarifa iliyiotolewa jana kwa vyombo vya habari na Ikulu.

Rais aliwataka polisi wa usalama barabarani kutokuwa waangalifu tu pale ajali inapotokea na kulegeza kamba baada ya tukio kwisha.

“Hili ni eneo ambalo litazidi kuwa tatizo siku hadi siku, kama hamtakuwa makini na kuonesha ushupavu kwa wanaovunja sheria na kutozingatia mahitaji ya chombo salama cha usafiri wa binadamu na mali zao wakati wote,” alisisitiza.

“Nawapa pole wafiwa wote, nawatakia waliojeruhiwa kupata ahueni haraka iwezekanavyo na kurudi katika shughuli zao za kila siku,” alisema.