BABU mwenye umri wa miaka 84, Richard Byerley, amevunja rekodi ya dunia kwa kuweza kupanda na kufika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro akiwa mtu mwenye umri mkubwa kuliko
wote waliowahi kukifikia kilele hicho.
Hatua hiyo, pamoja na kumfanya babu huyo kuweza kuingia kwenye rekodi ya Dunia ya Guinness, inamfanya pia kuvunja rekodi iliyowekwa na Mwingereza, Profesa mstaafu George Solt, aliyevunja rekodi hiyo mwaka 2010 kwa kupanda na kufika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro akiwa na umri wa miaka 82.
Byerley na wajukuu wake wawili walifika katika kilele hicho cha Mlima Kilinjaro kilichopo urefu wa futi 19,340, kabla ya jua kuchomoza Oktoba 6, mwaka huu. Mafanikio hayo ya Byerley, yamewavutia maelfu ya watu duniani ambao katika kumuenzi, wamefungua ukurasa
maalumu katika Sura Kitabu (Face Book) na kuuita “Mashabiki wa Richard Byerley" kwa anuani ya http://www.facebook.com/Richa rdByerleyKilimanjaro.
Akizungumza na Mwandishi wa Habari wa Kujitegemea anayeishi Bouder, Colorado, Karen Goodwin, Byerley alisema, “ Nafurahi kuona kuwa pamoja na umri wangu wa miaka 84 nimeweza kupanda hadi katika kilele cha Mlima Kilimanjaro na kurejea chini nikiwa na afya njema.
“Hata hivyo nikiri wazi kwamba kiukweli nilikuwa mpweke kwa kuwa kwa muda niliokuwa
Afrika sikuwa na mke wangu Beth ambaye nimeishi naye kwa miaka 63 tangu tufunge ndoa tukiwa na upendo wa hali ya juu na kamwe hatutatengana.
“Beth alipanda Mlima Kilimanjaro miaka 30 iliyopita, lakini nilipomshawishi tuje tena safari hii alinigomea, akaniambia ile mara moja aliyopanda ilikuwa inamtosha na hataki tena kufanya hivyo... sasa nimeelewa ni kwa nini mwenzangu aligoma kupanda tena Mlima Kilimanjaro katika umri huu.
“Ilituchukua siku sita kuweza kufika kileleni kupitia njia ya Machame, sikuweza kupata tatizo lolote la kiafya. Kwa hilo ninamshukuru Mungu, tatizo langu kubwa ilikuwa mikono yangu kufa
ganzi kutokana na baridi kali. “Tulikaa kileleni kwa muda kama wa dakika 30, tukipiga picha na kuangalia mandhari ya kileleni.
Niliambatana na wajukuu zangu Annie, mwenye umri wa miaka 29, na Bren, mwenye miaka 25, ambao ni mtu na dada yake ambao kwa siku zote hizo walizitumia kuzungumzia masuala ya familia yetu na kwa kweli tulifurahia siku zote sita.
“Tulifikia kileleni kabla ya jua kuchomoza Oktoba 6.Tuliondoka katika kambi ya mwisho saa 11:45 na kufika pale juu kileleni saa 12:15, alfajiri na kwa hiyo ilituchukua kama muda wa saa sita hivi kutoka kwenye ile kambi ya mwisho hadi kileleni.
“Kulikuwa na giza kubwa sana, kila kundi lilikuwa na taa ya kuwaongoza, kuna wakati nilitazama nyuma na kuona taa zikija nikajipa moyo kwamba kumbe sisi tulikuwa mbele zaidi. Nakumbuka kuna kundi moja lilitupita, lakini na sisi tuliyapita makundi ya watu wengine.
“Wakati tukipanda, ardhini kulikuwa na barafu ya ukubwa wa inchi kama mbili hivi na juu ya kilele tuliona theluji nyingi zaidi. Mwongozaji wetu alisema ni kawaida kukutana na theluji juu ya njia. Ni dhahiri kwamba mvua haikunyesha kule kileleni lakini kulikuwa na theluji ya hali ya juu kama unavyojua ni urefu wa futi 19,340.
“Ningesema ilikuwa ni juu ya nyuzi joto 15. Hakukuwa na upepo, lakini kulikuwa na matabaka ya mawingu chini yetu. “Wakati wa kushuka hakukuwa na tatizo kubwa kwani tuliweza kutembea maili zote nne hadi ilipo kambi ya mwisho kutoka juu ya kilele kwa muda wa saa tatu tu.
Mwongozaji wetu sana alipendekeza tukodi vijiti vya kutusaidia kuteremka mlima katika
baadhi ya maeneo, nakumbuka siku ya mwisho mimi sikutumia kabisa vijiti vile.
“Naweza kusema siku ya pili ndiyo ilikuwa siku ngumu zaidi katika safari yetu maana hakukuwa na njia ya uhakika, kuna wakati ilitubidi kubuni njia zetu wenyewe na kukumbana na matabaka ya mawe lakini tuliweza kufika kwenye kituo lakini tukiwa na uchovu mkubwa mwingi.
“Sasa inaonekana dhahiri kwamba mimi ndiye mtu mkongwe zaidi kuweza kupanda Mlima Kilimanjaro hadi kileleni. Wakati nikinunua safari hii kwenye mnada wa kule Sun Valley, Idaho kule Marekani, Sikujua chochote kuhusu kumbukumbu za watu waliowahi kupanda Mlima Kilimanjaro, niliona kama ni moja ya safari nzuri kwangu.
“Lakini Robin Paschall, mmiliki wa kampuni ya Utalii ya Adventures baada ya kufika pale aliniambia kama nitaweza kufika kileleni nitakuwa mtu mkongwe wa kwanza duniani kuweza kufika kileleni katika umri mkubwa. Sikuweza kufahamu kama nitaweza hadi pale nilipojaribu na kuweza.
“Watoto wangu wanne wenye umri wa kati ya miaka 53 na 60 walikuwa 'bize’ na kazi, na Beth yeye alisema najisikia kufanya hivyo tena, lakini wajukuu zangu Annie Na Bren ambao walikuwa na maumivu ya kichwa ya muda mrefu kabla ya kupata nafuu walikuwa mstari wa mbele kujitolea kuongozana na mimi.
“Nilihamasika sana na waongoza wageni na wabeba mizigo. Walikuwa wakibeba mizigo mingi na mizito na kupanda nayo mlimani bila wasiwasi. Walibeba vitu kama mahema na vyakula na kutuongoza huku wengi wao wakiwa wamevaa viatu vya kawaida kama vile vinavyovaliwa mitaani.
“Wapanda milima mara nyingi huvua buti na viatu vyao na kuwakabidhi wabeba mizigo. Beth alifanya hivyo miaka 30 iliyopita, alisema baada ya kupanda miguu ilikuwa na vidonda hivyo hakutaka kuona buti hizo kamwe tena.
Baada ya kufika chini niliwapa wapagazi zawadi mbalimbali. Kimsingi wapagazi wanaendesha maisha yao kwa kutegemea zawadi na pesa kufanya maisha yao kuwa mazuri ingawa wanafanya kazi kubwa sana.
“Watu waliniuliza najisikia vipi baada ya kuvunja rekodi ya dunia na kuingia katika kumbukumbu ya rekodi za Guinness. Niliwaambia mimi bado ni mtu yule yule kama nilivyokuwa mwanzo.
Niliwaambia ni kama vile mtu anaponunua nyumba au gari jipya lakini bado anabakia kuwa mtu yule yule. “Tulisafiri kwa saa 18 katika ndege tukirejea nyumbani kutoka Afrika, na tulipofika nyumbani Beth aliniandalia pati kwa ajili ya kunipongeza.
Watu wengi walinihoji nini siri ya mimi kuwa na afya njema kiasi cha kuweza kupanda mlima
mrefu Afrika, Mlima Kilimanjaro na mimi niliwajibu ni kutokana na kuwa na mwanamke bora kama Beth ambaye ananipa kila kitu kizuri ili kulinda afya yangu.
Huyo ndiye Richard Byerley, mzee mwenye umri wa miaka 84 ambaye ameweka rekodi ya dunia baada ya kufika kileleni mwa mlima mrefu kuliko yote Afrika na wa pili kwa urefu duniani, Kilimanjaro.
Je, kuna atakayevunja rekodi ya mzee huyo ambaye amekuwa mithili ya balozi wa Tanzania na Mlima Kilimanjaro kote duniani? Bila shaka ni jambo la kusubiri na kuona.
0 Comments