Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi, David Jairo.

*Ni kwa kuzichangisha taasisi kinyume na taratibu
*Ngeleja, Luhanjo, CAG nao yaagizwa wawajibishwe
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi, David Jairo ametiwa hatiani kutokana na kuchangisha fedha kutoka taasisi nne zilizoko katika wizara hiyo kinyume cha taratibu.

Kamati Teule ya Bunge imependekeza kwa serikali imchukulie hatua za kinidhamu kwa matumizi mabaya ya madaraka, ukusanyaji na kutumia fedha za serikali kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za fedha za umma.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati Teule iliyoundwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, Agosti 26, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ramo Makani, alisema kuwa kamati yake pia imependekeza watumishi wote wa Wizara ya Nishati na Madini waliotajwa katika taarifa hiyo kushiriki kwa namna mbalimbali katika mchakato wa uchangishaji na matumizi ya fedha za umma wachukuliwe hatua.

Kamati ilisema kuwa uchunguzi wake ulibaini kuwa kanuni ya 4(4) ilikiukwa. Kanuni hiyo inasema kuwa kama zinatakiwa fedha za bajeti za ziada zinapaswa kuidhinishwa na Bunge. Ilisema mtiririko wa maelezo ya wizara kuhusu uchangishaji ulitakiwa kuishia katika vifungu vya bajeti ya wizara yenyewe na mabadiliko hayo yalipaswa kupata idhini ya Waziri wa Fedha badala ya kuamua kuzichangisha taasisi.

Aidha, imependekeza kwamba Serikali imchukulie hatua zinazofaa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kwa maelezo kuwa kwa mujibu mujibu wa Mwongozo wa Baraza la Mawaziri, Waziri ndiye Msimamizi Mkuu wa wizara, hivyo suala la uchangishaji halikupaswa kufanyika bila yeye kufahamu.

Kamati Teule pia imependekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kwa maelezo kuwa kwa makusudi aliamua kumsafisha Jairo kwa kuficha ukweli wa Taarifa ya Ukaguzi Maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuamua kwamba Jairo hakuwa na kosa la kinidhamu, kitendo ambacho kimeupotosha umma wa Watanzania.

Kamati ilisema kuwa kitendo cha Luhanjo kutoa taarifa ya uchunguzi kwa umma kupitia vyombo vya habari wakati Bunge halijapewa taarifa kimeathiri dhana ya haki na madaraka ya Bunge kisheria.
“Hata hivyo, kwa kuwa suala hili lilianzia bungeni, na kwa kuwa kulikuwepo na mawasiliano kati ya Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi kabla ya kuanza kwa mchakato wa uchunguzi wa wali, hivyo basi Katibu Mkuu Kiongozi alikuwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba Bunge kupitia kwa Waziri Mkuu linapata taarifa ya matokeo ya uchunguzi kabla hajaitoa kwa vyombo vya habari,” alisema Mkani.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh, naye amekutwa na hatia na Kamati Teule imependekeza kuwa serikali ichukue hatua zinazofaa dhidi yake.

Makani alisema kuwa Kamati Teule imesikitishwa sana na jinsi CAG Utouh alivyoshindwa kutekeleza wajibu wake kikamilifu, hususan katika kutoa ushauri na hitimisho katika ripoti yake na jinsi alivyotoa taarifa katika vyombo vya habari na kumsafisha Jairo.

“Kwa kufanya hivyo, ameshindwa kulisaidia Bunge na umma kwa ujumla, badala yake amekuwa ni sehemu ya kuficha maovu,” alisema Makani huku akishangiliwa na wabunge.

Iliongeza kuwa kupitia taarifa ya CAG, Kamati Teule imebaini kuwa licha ya kuonyesha upungufu, wa aina mbalimbali katika kuendesha zoezi la uchangishaji na matumizi ya fedha hizo, taarifa hiyo haikuweza kuweka bayana kama uchangishaji huo ulikuwa halali au vinginevyo katika kutoa ushauri na hitimisho.
Kamati Teule imependekeza kwamba Bunge likemee kwa nguvu zote utaratibu wa uchangishaji huo na Wizara ya Nishati na Madini na kwamba uchangishaji wa fedha wa aina yoyote lazima uzingatie Sheria, Kanuni na Taratibu wa fedha.

Ili kudhibiti uchangishaji na matumizi ya fedha za umma, Kamati Teule imependekeza Sheria, Kanuni na Taratibu zilizoko zifanyiwe marekebisho ili kutoa nafasi kwa Makatibu Wakuu kuwashirikisha Mawaziri katika maamuzi ya kiutendaji hasa katika matumizi ya fedha, hatua ambayo itawapa Mawaziri fursa ya kutekeleza vizuri zaidi majukumu yao wakiwa kama wasimamizi wakuu wa maamuzi na shughuli za serikali wizarani.

NIDHAMU KWA WATEULE WA RAIS

Kuhusu nidhamu kwa wateule wa Rais, Kamati Teule imeona kuwa si vema suala hilo kuacha mikononi mwa mtu mmoja kama ilivyo sasa katika Sheria ya utumishi wa Umma na kupendekeza kwamba mamlaka ya Nidhamu kwa watumishi wa umma wanaoteuliwa na Rais inaposhughulikia masuala ya nidhamu ifanye hivyo kwa kumuarifu Rais ambaye ni mamlaka ya uteuzi na Waziri Mkuu ambaye ni msimamizi wa siku hata siku wa kazi na shughuli za serikali au serikali iunde chombo maalum cha kushughulikia masuala ya nidhamu kwa watumishi wa umma wanaoteuliwa na Rais.

Kabla ya kutoa mapendekezo na maoni yake, Makani alieleza jinsi Kamati Teule ilivyofanya kazi yake kwa kuwahoji mashahidi 146 na mambo ambayo iliyagundua.
Kuhusu uchangishaji wa fedha ambao ulidaiwa kufanywa na Jairo, alisema kuwa matokeo ya uchunguzi huo yamebainisha kwamba utaratibu wa wizara kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasilisha Bajeti yake bungeni haukuwa wa kawaida na haukujengwa katika misingi yoyote ya kisheria na pia, fedha zilizokusanywa zilitumika kwa ajili ya matumizi ambayo yasingehitaji uchangishaji kwa sababu yangeweza kugharimiwa na kasma zilizopo za wizara.

Kuhusu Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), alisema kuwa ilichangia Sh.milioni 50 kutoka kasma ya mapato ya gesi ya serikali na kwamba kasma hiyo ni mapato ya serikali na siyo kasma ya kuchangia wizara kuwasilisha hotuba ya bajeti.

Alisema Kamati ilipitia kanuni za fedha za TPDC, 2008 na Mwongozo wa ukomo wa Mamlaka kuidhinisha malipo mbalimbali na kubaini kuwa matumizi yote ambayo hayajapitishwa katika bajeti yatafanyika kwa idhini ya Bodi tu.

Hata hivyo, alisema katika mahojiano na watendaji wa TPDC, Kamati ilibaini kuwa shirika hilo lililazimika kuchangia fedha hizo bila idhini ya bodi kama inavyotakiwa na kanuni ili kutii maagizo ya Jairo. Kwamba TPDC walilazimika kuchanga kinyume cha utaratibu kwa kuhofia kuitwa wakaidi kutokana na uzoefu waliokwishaupata siku za nyuma.



TANESCO
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lilitumia kasma ya michango ya kijamii na ada za uanachama kuchangia Sh. milioni 40. Kasma hiyo ilikuwa na Sh. milioni 200 chini ya mamlaka ya Mkurugenzi Mtendaji.

Hata hivyo, Makani alisema kuchangia wizara kwa ajili ya kuwasilisha bajeti siyo shughuli mahususi iliyolengwa katika kuisaidia jamii wala siyo ada ya uanachama katika wizara na kwamba maoni ya kamati ni kuwa fedha hizo hazikutumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa.

EWURA

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Madini iliombwa kuchangia Sh. milioni 40. Makani alisema mamlaka hiyo haikuwa tayari kuchangia fedha hizo, badala yake waliomba wachangie kwa kulipia gharama ya vyakulana vinywajikwa gharama ya Sh. milioni 9.7

Alisema kutokana na mahojiano na watendaji wa Ewura, msingi wa ombi hilo la kuchangia chakula na tafrija ni kuwa maombi ya Sh. milioni 40 kutoka wizarani hayakuainisha mchanganuo wa matumizi.

Alisema ewura walipima wenyewe na kutumia busara kwamba badala ya kupeleka fedha hizo wizaraniwatagharamia chakula na tafirija wao wenyewe na kwamba busara hiyo ilisaidia kuokoa Sh. milioni 30.

REA

Mamlaka ya Nishati ya Umeme Vijijini (Rea) ilichangia Sh. milioni 50 kutoka kasma ya kuandaa mpango kazi. Kasma hiyo ilikuwa na Sh. Milioni 37.5 hata hvyo, Aprili 15, 2011 kasma hiyo ilikuwa na bakaa ya Sh. milioni 7.7 tu, lakini ikaongezewa Sh. milioni 75 kwa utaratibu wa kuhamisha fedha hivyo kufanya kasma kuwa na Sh. milioni 82.9 hatua ya kuchangia Sh. milioni 50 wakati katika kipindi kifupi kilichotangulia Rea ilichangia Sh. milioni 22 ni kufanya jumla ya michango kwa wizara kuwa Sh. milioni 72kutoka katika kasma iliyotengewa Sh. milioni 82.9, inaonyesha wazi kuwa kasma hii isingeweza kutekeleza jukumu lililokusudiwa kwani ilibaki na Sh. milioni 9.7 ambazo ni sawa na asilimia 13 ya kasma yote.

Makani alisema Kamati ilipitia mwongozo wa REA wa matumizi ya fedha ambao umezingatia sheria na kanuni mbalimbali zikiwemo za Rural Energy Act ya mwaka 2005, Sheria ya Fedha za Umma na kanuni zake na Sheria ya manunuzi ya Umma na kanuni zake na kubaini kuwa kifungu cha 16.4 cha Mwongozo wa Fedha na Matumizi kinachohusu shughuli au matumizi ambayo hayakupangwa kinaweza kutumika vibaya kwa kuidhinisha matumizi yasiyo na tija.

Makani alisema kuwa mahojiano na uchambuzi wa nyaraka za bajeti na matumizi ya wizara kuhusu fedha zilizochangishwa, Kamati Teule ilibaini kuwa mahitaji halisi ya maandalizi ya hotuba ya bajeti yalikuwa Sh. 206,042,000 ambayo Jairo aliridhia. Kati ya Sh. 206,042,000 zilizohitajika, Sh. milioni 35.5 zilitoka kifungu cha Project Cordination and Monitoring cha wizara, hivyo wizara ilibaki na upungufu wa Sh. 171,542,000.
Kwa mujibu wa Makani, kwa lengo la kuziba upungufu huo, Juni 25, 2011, Jairo alituma Sh. 171,542,000 kwa njia ya TISS Bo BOT kwenye akaunti namba 5051000068 ya GST Dodoma na kwamba fedhan hizo zilipokelewa na na GST Dodoma kwa stakabadhi namba 02428 ya Juni 25,2011. Alisema kufikia Juni 25, 2011 wizara ilikuwa tayari ina fedha za kutosha kuwasilisha hotuba ya bajeti bungeni bila kuhitaji michango kutoka kwenye taasisi.

“Lakini pia, hiyo tarehe 25 Juni, 2011 ni siku tano tu baada ya wizara kutuma barua za kuomba michango kwenye taasisi na ni siku 20 kabla ya wizara kuwasilisha hotuba ya bajeti yake bungeni,” ilieleza taarifa ya Kamati Teul e yenye kurasa 150 na kuongeza:

“Hivyo wizara ilikuwa na muda wa kutosha kuzuia michango isiendelee kama ingetaka kufanya hivyo, baada ya kuona fedha zilizokuwepo hadi wakati huo zilikuwa zinatosha kwa maandalizi na uwasilishaji wa bajeti yake.”

Vile vile, Kamati ilibaini kuwa wizara ilipeleka Dodoma watumishi 243 ambao ni ongezeko la asilimia 400 ya watumnishi waliodhinishwa na Katibu Mkuu ambao walikuwa 61 na kusababisha matumizi makubwa.

Kamati Teule ilisema kuwa imeridhika kuwa suala lililoibuliwa na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo, ilikuwa ni hoja ambayo kwa uzito wake na kwa hisia zilizotawala mjadala, huo, serikali ilitakiwa kuifanyia kazi na kutolea taarifa ya utekelezaji bungeni.

NGELEJA, MALIMA WAGUSWA
Kamati Teule imebaini kwamba Waziri Ngeleja na Naibu Wake, Adam Malima walilipwa posho ya entertainment ya Sh. 500,000 kwa kila mmoja kwa siku nane hivyo kila mmoja kulipwa Sh. 4,000,000 kinyume na taratibu za serikali.

Miongoni mwa watu waliofika kwa Kamati Teule wengine kuandikiwa kwa ajili ya kutoa maoni ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya; Spika wa Bunge Mstaafu, Pius Msekwa; Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema; Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), John Cheyo; Luhanjo; CAG Utouh; wabunge, mawaziri na wabunge wa bunge la Uingereza.

Mbali na Makani wajumbe wengine wa kamati hiyo walikuwa Martha Umbulla (Viti Maalum-CCM); Gosbert Blandes (Karagwe-CCM); Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema) na Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF).

   CHANZO CHA HABARI HII GONGA MAANDISHI HAYA