Didier Drogba atafanyiwa upasuaji kuondoa skrubu zilizofungwa mkononi mwake katika upasuaji uliofanyika mwaka jana.
Chelsea itatumia nafasi ya Drogba kufungiwa kucheza mechi za Ligi ya England ili aweze kufanyiwa upasuaji huo.
Mechi ya Jumanne ya Ligi ya Ubingwa wa Ulaya ambapo Chelsea itapepetana na Genk, Drogba hatakuwemo katika kikosi hicho na atakuwa amepona tayari kuikabili Liverpool tarehe 20 mwezi wa Novemba.
Mechi ijayo ya Chelsea itakuwa dhidi ya Blackburn siku ya Jumamosi tarehe 5 mwezi wa Novemba, lakini mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast hataweza kucheza mechi hiyo baada ya kuoneshwa kadi nyekundu katika mechi dhidi ya Queens Park Rangers tarehe 23 Octoba.


Villas-Boas meneja wa Chelsea amesema: "Tunachukua nafasi hii ya kusimamishwa kwake katika mechi za ligi ya England na ijayo ya kimataifa ili afanyiwe upasuaji kuondoa skurubu sita kati ya nane zilizofungwa mkononi mwake."
Drogba alivunjika mfupa katika kiwiko chake cha mkono mwaka 2010, awali kukawa na wasiwasi asingeweza kucheza mashindano ya Kombe la Dunia, lakini upasuaji aliofanyiwa uliokwenda vizuri ulimuwezesha acheze.

Drogba katika mechi saba alizocheza za Ligi Kuu ya England msimu huu amefunga bao moja tu na bado msimu huu hajakanyaga uwanjani katika mechi yoyote ya Ligi ya Ubingwa wa Ulaya.