Maafisa wawili waandamizi katika utawala wa kijeshi nchini Misri wameomba radhi kufuatia mauaji ya waandamanaji yanayoendelea katika mji mkuu Cairo na miji mingine nchini humo.

Majenerali hao wamejitokeza katika televisheni ya serikali wakitoa salaam za rambirambi kwa wananchi wa Misri.

Hii ni mara ya kwanza kwa watawala wa kijeshi kuomba radhi tangu mgogoro uanze nchini Misri.

Serikali itatangaza leo namna wanavyopanga kuendelea na shughuli za uchaguzi wa ubunge unaotarajiwa kuanza Jumatatu ijayo.


Ujumbe wa majenerali hao ulionekana kuwa wa kuwapa moyo watu kinyume na awali ambapo walionyesha ukali na tarayi kukabiliana na upinzani hususan kwenye hotuba ya kiongozi wa baraza tawala la jeshi Field Marshall Tantawi.

Wakati huu wanajeshi hao wametuma rambirambi kwa raia wa Misri pamoja na kuomba msamaha kwa niaba ya jeshi nzima kutokana na maafa yaliyotokana na vurugu za maandamano.

Pia wamewasihi raia kutofananisha utawala wao na enzi ya rais aliyeng'olewa madarakani Hosni Mubarak.Wamesema hao ni tofauti kabisa kwani hawanuii kutwaa madaraka au kusalia uwongozini.

Vurugu zimetulia usiku kucha katika medani ya Taharir japo maelfu ya waandamanaji wamekita kambi na hkuna dalili kwamba huenda wameridhia msamaha walioombwa na jeshi.