BAADA ya Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan kutishiwa kuuawa, ni wazi wauaji wameanza kazi, kwani hivi karibuni, walivamia gari lake, wakalishambulia kwa silaha mbalimbali na kusababisha uvunjifu wa kioo.
Kama si ujasiri wa dereva kuongeza mwendo kuwakimbia watu hao, pengine habari ingekuwa nyingine.
Gari la Azzan, BMW lenye namba za usajili T 749 BBK lilishambuliwa Jumapili ya Novemba 20, mwaka huu saa 12:30 jioni katika Kijiji cha Chinangali, kilometa 2 kabla ya kufika eneo la Chalinze (ya Dodoma), mkoani humo.
Akizungumza na waandishi wetu jijini Dar, Jumatatu iliyopita, Shaweji Mkumbula ambaye alikuwa dereva wa gari hilo, alisema mheshimiwa Azzan hakuwepo ndani ya gari hilo, ila yeye na watu wengine wawili, Fabian Sambi na Rafael Maumba walikuwa wakitokea Dodoma kwenda Dar.
Alisema, walipofika eneo hilo walisikia mshindo mkubwa kwenye kioo cha nyuma upande wa dereva lakini hawakusimama kwa kuhofia usalama wao.
Alisema baada ya kufika umbali mrefu walikagua gari hilo, walipokigusa kioo cha dirisha la nyuma upande wa kulia kilimwagika.
Akasema: “Tulimpigia simu mheshimiwa (Azzan) kisha tukaenda kuripoti katika Kituo cha Polisi cha Dumila (Dodoma) na kupewa RB/ Dum/IR/911/2011.
Siku za hivi karibuni, mhesimiwa Azzan alilalamikia kutishiwa maisha kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu na watu wasiojulikana.
Alisema, watu hao walimwambia lazima wamuue, hivyo kumpa hofu ambayo ilimfanya aende kuripoti kwenye vyombo vya usalama.
Akizungumza na gazeti hili juzi (Jumanne), Azzan alisema, anaamini watu waliolishambulia gari lake ni wale waliomtumia meseji ya kumtishia kifo.
Aliongeza kuwa wabaya wake hao walijua yeye alikuwa miongoni mwa watu waliokuwemo ndani ya gari.
Azzan alisema, anaamini Mungu ataendelea kumlinda siku zote za maisha yake. “Naamini watu waliolishambulia gari langu ni wale walionitumia ujumbe wa simu kuwa wataniua, wao walijua nimo ndani ya gari, kumbe sivyo, Mungu ananilinda,” alisema Azzan.
Mbunge huyo amekuwa katika mgogoro na baadhi ya wana CCM wenzake, hususan viongozi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam.
Mgogoro wa Azzan na viongozi wa CCM, ulianza pale alipochokoza dhana ya kujivua gamba, akitaka viongozi wa chama hicho Dar wang’oke kwa sababu walisababisha kupoteza majimbo mawili na kata nyingi katika Uchaguzi Mkuu 2010.
Sakata la Azzan, lilifika pabaya zaidi alipoanza kusukiwa mpango wa kuwekewa madawa ya kulevya kwenye gari ili akamatwe nayo, tukio ambalo aliliripoti Idara ya Usalama wa Taifa kisha akaanza kuishi kwa tahadhari ya hali ya juu.
CHANZO CHA HABARI
0 Comments