WATANZANIA watakaonunua nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa bei ya Sh milioni 25 kupitia mikopo ya benki saba zilizoingia mkataba na shirika hilo, watalazimika kulipa kati ya Sh milioni 63 na 75, kutokana na riba ya asilimia 15 na 19 itakayotozwa kwa miaka 15.

Hesabu hizo ni kwa mujibu wa Benki ya Azania, itakayotoza riba ya kuanzia asilimia 15, na KCB Bank (T) Ltd itakayotoza riba isiyopungua asilimia 19.

Benki nyingine zilizosaini makubaliano ya kutoa mikopo hiyo ya nyumba; BOA, NMB (T) Ltd, EXIM, CBA na NBC, pia zitatoza riba ya kati ya asilimia 15 na 20. 


Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana, wahusika wa mikopo ya nyumba katika benki hizo walisema Sh milioni 25 inayotangazwa na NHC ni fedha ambayo benki hizo zinapaswa kulilipa shirika hilo, kama malipo ya jumla ya nyumba moja, ambayo wateja hao wanapaswa kuyarejesha kwa benki husika pamoja na riba.

Ofisa Mikopo wa Azania, tawi la Dar es Salaam, Gulshan Saleh, aliiambia HABARILEO ofisini kwake, kuwa mteja atakayepewa na benki hiyo mkopo wa nyumba wa Sh milioni 25, kwa riba ya asilimia 15 kwa miaka 15 (miezi 180) atapaswa kurejesha Sh 349,896.78 kila mwezi, kwa kipindi hicho.

Kwa maelezo ya Saleh, kiasi hicho ni jumla ya riba ambayo ni Sh 312,500, pamoja na makato ya msingi ya Sh 37,396.78.



“Kutokana na mchanganuo huo, hadi kumalizika kwa mkopo, mteja atakuwa amelipa Sh. 2,981,420.34; Sh milioni 25 ikiwa ni marejesho yaliyolipwa na benki kwa NHC, na Sh 37,981,420.78 inayobaki kwa benki kama marejesho ya gharama za mkopo na faida,” Saleh alisema.

Kwa upande wa KCB (T) Ltd, ofisa aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa gazetini, alisema riba yao kwa mikopo hiyo ya nyumba ni asilimia 19, ambayo hawatarajii kuipunguza kutokana na sababu mbalimbali.

Alifafanua, kuwa mteja atakayepewa mkopo wa nyumba wa Sh. milioni 25 atailipa KCB Sh 420,719.01 kwa mwezi, ambayo ni jumla ya makato ya msingi na riba.

“Kwa hesabu hizo, hadi kukamilisha mkopo wake wa miezi 180 (miaka 15) katika benki yetu, mteja atakuwa amelipa Sh. 75,729,421.8 , ambapo Sh. milioni 25 zitakuwa ni marejesho kwa fedha ambazo NHC itakuwa imelipwa kwa niaba yake, wakati Sh. 50,729,421.8 ni gharama ya mkopo na faida,” alisema ofisa huyo.

Kutokana na hesabu hizo, ambazo wahusika walieleza kuwa ni za awali, mfanyakazi anayeweza kununua nyumba ya Sh milioni 25 kupitia mkopo wa benki wa muda huo mrefu ni mwenye kipato kinachoweza kuruhusu theluthi mbili ya makato kwa ajili ya mkopo huo na kubakiwa na thekuthi moja ya kuendeshea maisha.

Hiyo ni baada ya makato mengine ya lazima, kama vile NSSF, PAYE na mengineyo kama yapo.