MASTAA wa filamu ‘the highest level’, Vincent Kigosi ‘Ray’ na Steven Kanumba ‘The Great’, (pichani) urafiki wao uliofanya waitane maswahiba, umeingia doa na sasa kuna bifu zito linalotokota.

Uchunguzi wa Amani umebaini kuwa chanzo cha bifu la Ray na Kanumba ni magari yao ya kifahari ambayo wameyanunua hivi karibuni.

Gazeti hili limebaini kuwa kuna watu wametengeneza makundi mawili na kutengeneza vijembe kisha kuvirusha kwa mastaa hao, vitendo ambavyo vimesababisha uhasama.

Chanzo chetu kilisema: “Watu ndiyo wamewafanya Ray na Kanumba wagombane. Kuna kundi lilipika maneno kwamba Ray analiponda gari la Kanumba, vivyo hivyo lingine likadai Kanumba analiponda gari la Ray.


“Hayo maneno ndiyo yamezaa bifu kati ya Ray na Kanumba. Hawatazamani vizuri kwani kila mmoja anaamini mwenzake anamponda.
“Hakuna urafiki na hata wakienda kwenye shughuli yoyote hawakaribiani, wanakaa mbalimbali.”

MADONGO YANAYOPOROMOSHWA
Uchunguzi wa Amani umebaini kuwa madongo anayopigwa Ray ni haya;

MOSI: Gari lake aina ya Toyota Land Cruiser V8 halina thamani ya shilingi milioni 60 kama alivyotangaza.

PILI: Yeye si chochote mbele ya Kanumba mwenye gari aina ya Toyota Lexus lenye thamani ya shilingi milioni 78.TATU: Hana fedha kumfikia Kanumba kwa sababu ‘bwa’mdogo’ wa Usukumani anapiga dili nyingi zinazomuingizia ‘mapene kibao’ nje ya fani ya filamu.

Amani pia limebaini kuwa Kanumba anafumuliwa kwa madogo haya;

MOSI: Gari lake limechoka, ni kuukuu. Hata herufi za namba zake za usajili (AER) zinaonesha ni la zamani na amenunua kwa mtu, wakati la Ray ni mpya kabisa na amelisajili mwenyewe likiwa na herufi BTZ.

PILI: Amedanganya thamani ya gari lake kwamba amenunua shilingi milioni 78, badala yake amenunua kwa mtu shilingi milioni 35.



TATU: Ni kawaida yake kumuiga Ray, ndiyo maana amenunua Lexus baada ya Ray kuvuta V8. Hata biashara, alianza Ray na kampuni ya filamu ya RJ ndipo Kanumba naye akasajili yake aliyoiita Kanumba The Great.

NNE: Kanumba ni ‘chamtoto’ kwenye fani, kwani amefundishwa kazi na Ray na hata umaarufu alionao unatokana na kupikwa kitaalamu na bosi huyo wa kampuni ya RJ.

RAY, KANUMBA WATHIBITISHA
Amani limethibitishiwa kuwa madongo hayo yanapopelekwa kwa Ray, huelezwa yamesemwa na Kanumba, hivyo kukuza bifu.

Kadhalika, Amani limeelezwa kuwa Kanumba anapofikishiwa madongo yake, huambiwa aliyesema ni Ray, jambo ambalo limekuwa sawa na kutupa kijinga cha moto kwenye pipa la petroli.Ray alipozungumza na gazeti hili, alikiri kuwepo hali ya kutoelewana kati yake na Kanumba, akafafanua:

“Yalipita maneno baada ya mimi kununua gari langu V8 na yeye kununua lake.

Ni maneno ya watu yakichangiwa pia na ulevi. Watu wakishalewa usiku, linasemwa hili na lile ndiyo yakasababisha mgogoro.

“Kwa upande wa maisha yangu, sipendi bifu. Mimi ni mtumishi wa Mungu, Kanumba ni mdogo wangu, tutakaa na kumaliza haya maneno. Ninaponunua gari au kitu chochote kile ni kwa matumizi yangu na siyo kushindana na mtu.”Kwa upande wa Kanumba, aliliambia Amani: “Hayo maneno yapo na anayesema gari langu ni shilingi milioni 35 aende ‘yadi’ akaangalie Lexus nyeusi linauzwa bei gani. Mimi ni The Great na sishindani na mtu.”
CHANZO