KATIBA mpya ya Tanzania itaandikwa na Watanzania wenyewe kwa kupitia maoni yatakayotolewa nao kwa Tume itakayoundwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Rais Jakaya Kikwete alipozungumza na Taifa
kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema kila Mtanzania atapewa fursa ya kutoa maoni yake kwa Tume ambayo ataiunda
kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar mara Muswada wa marekebisho ya Katiba uliopitishwa
jana na Bunge la Jamhuri utakapokuwa umesainiwa.

Alisisitiza, k w a m b a T u m e haitaacha kusikiliza maoni na hoja ya kila mtu atakayependa kushiriki kuchangia, lakini hayo yatafanyika kwa kuzingatia sheria.

“Katiba iliyopo itafuatwa, kwa sababu ndiyo iliyopo kwa sababu kubadili Katiba lazima ya zamani iwepo, hivyo itafuatwa na kuzingatiwa katika mchakato mzima wa kupata Katiba mpya,” alisema Rais.

Tume kuteuliwa na Rais Juu ya malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wanaharakati pamoja na wanasiasa, hususan wa upinzani kwamba yeye hastahili kuunda Tume ya kusimamia mchakato wa kuandika Katiba, Rais alishangaa.

Alisema hii si mara ya kwanza kwa Rais kuunda Tume kama hiyo, kwa sababu hata waliomtangulia walipata kufanya hivyo akitolea mfano wa Rais wa Kwanza Mwalimu Nyerere ambaye aliunda tume kama hiyo mara tatu; mwaka 1963, 1964 na 1965

Akifuatiwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ambaye aliunda mara moja mwaka 1992 chini ya Jaji Francis Nyalali na Benjamin Mkapa mara moja ya Jaji Robert Kisanga.



Alisema Katiba iliyopo inampa mamlaka ya kuuda Tume hiyo, ambayo alisema itajumuisha watu wa kada mbalimbali na kufuatiwa na Bunge Maalumu la Katiba, ambalo litajumuisha wanasiasa wakiwamo wabunge, wawakilishi na watu wengine 300.

Kuhusu hoja kwamba Zanzibar isipewe fursa sawa na Tanzania Bara, Rais aliponda hoja hiyo, akisema udogo wa nchi si hoja na kinachotakiwa ni ushirikishi kwa usawa.

“Hizi ni nchi huru zenye hadhi sawa-udogo si hoja, Shelisheli ina watu 84,000, lakini ni Taifa huru, hivyo mkiamua kuungana nayo, lazima mnakuwa na haki sawa pia,” alisema Rais.

Katiba ya sasa si mbaya Pamoja na kutaka kuja na Katiba mpya, lakini alisema Katiba ya sasa si mbaya, kwani imewalea Watanzania kwa muda mrefu katika mazingira ya amani na utulivu na kupiga hatua kubwa ya maendeleo kuliko ilivyokuwa miaka 50 iliyopita.

“Tunachotaka kukifanya sasa ni kuhuisha Katiba itakayofanana na Tanzania ya sasa. Katiba ya miaka 50 ijayo ambayo itaendelea kudumisha amani na utulivu,” alisema.

Alisema katika mchakato huo, kuna mambo ambayo yatatakiwa kujadiliwa na hasa kulindwa, kwa kuwa ndizo tunu za Taifa.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuwapo kwa nchi na mipaka yake; Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; Bunge; Mahakama; umoja; mshikamano na usalama; haki za binadamu; usawa mbele ya sheria; uhuru wa kuabudu na kuaminiana.

Alisema hayo yatazungumzwa kwa maana ya kulindwa na si kutaka kubomolewa, kuvunjwa au kukiukwa.

Akifafanua kuhusu kusomwa kwa Muswada huo bungeni, Rais alisema Muswada wa Katiba ulisomwa mara ya kwanza bungeni, ukachapwa katika Gazeti la Serikali siku 21 kabla ya
mkutano mwingine wa Bunge na kuwasilishwa katika Kamati ukajadiliwa na kupewa wadau ambao nao walichangia.

Kamati ilipomaliza kuujadili na wadau kuchangia, ukarejeshwa tena bungeni na kusomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa pia na Bunge na kisha kurekebishwa na kupitishwa na kusomwa mara ya tatu pale Katibu wa Bunge aliposoma taarifa ya Muswada
kupitishwa.

“Watu wanataka kupotosha tu, Muswada huu kila ulikopitia ulijadiliwa na tumeona mchango mkubwa wa majukwaa yaliyoundwa kuujadili na mikutano mbalimbali ya hadhara …
simu zilitumika, mitandao … kilichokosewa ni kipi?” Alihoji.

“Kwa kuwa Bunge linataka Tume iundwe na kuanza kazi Desemba mosi … zimebaki kama siku 12, tutaufanyia kazi, mimi na Rais wa Zanzibar tutaunda Tume na mwakani kazi ya wananchi kutoa maoni ifanyike na ili ifikapo mwaka 2014 wakati tunasherehekea miaka 50 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuwe na Katiba mpya … na uchaguzi wa 2015 ufanyike chini ya Katiba mpya,” alisema Kikwete.

Aliahidi kuwa watachagua watu wanaostahili kuunda Tume na si kwa kutumia urafiki wala kujuana na mtu bali weledi utazingatiwa.

Amshangaa Mbowe Rais alishangaa malalamiko yanayojitokeza hivi sasa juu ya mchakato huo kiasi cha baadhi ya vyama kukataa kuchangia bungeni, huku akimtaja kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Chadema), ambaye alimpongeza Rais
kwa kuruhusu mchakato wa Katiba mpya na sasa amegeuka.

Aliwataka wanasiasa na wanaharakati kuacha kupotosha wananchi kwa kutumia vibaya dhana ya nguvu za umma, huku jambo jema la Katiba mpya likiwa linasubiriwa na wengi.

Alisisitiza, kuwa Serikali haijakosea popote wala haijafanya kinyume cha sheria kutokana na
mchakato wa Muswada wa Katiba hiyo, hata kusababisha tuhuma na malalamiko yanayojitokeza hivi sasa.

Awali akizungumzia hali ya uchumi, Rais alisema matatizo yaliyopo hivi sasa ni matokeo ya hali mbaya ya uchumi duniani, huku akisema hali ya uchumi katika mataifa makubwa imetetereka.

“Huko ndiko yaliko masoko, watalii, mitaji ya uwekezaji na vifaa mbalimbali vya viwanda vyetu hivyo kukitikisika nasi tunatikisika … dola ya Marekani hivi sasa imeimarika ikilinganishwa na euro ya Ulaya hivyo kuathiri uchumi.

“Bei ya mafuta duniani nalo ni tatizo na imesababisha bei ya chakula na bidhaa zingine kupanda … hiyo ni pamoja na sera za kifedha kubadilika, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inachukua hatua za kukabiliana na hali hiyo,” alisema Rais.

Alisema kama mataifa makubwa yatarekebisha uchumi wao, mataifa madogo ikiwamo Tanzania nayo yataokoka.

Alitolea mfano wa mfumuko wa bei ambao Oktoba mwaka jana ulikuwa asilimia 4.2 lakini mwezi huo huo mwaka huu ukafikia asilimia 17.9.

Alisema hali hiyo iko pia katika nchi nyingine za Afrika Mashariki

Akifafanua kuhusu mafuta, alisema utaratibu uliopendekezwa na kukubaliwa nchini wa wafanyabiasharakuagiza mafuta kwa pamoja, utasaidia kurekebisha hali na unatazamiwa
kuanza mwezi ujao.                     KUTOKA