SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limewasilisha ombi la dharura kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) la kuidhinishiwa ongezeko la bei za huduma ya umeme kwa wastani wa asilimia 155 ya bei ya sasa.

Ongezeko hilo linalotarajiwa kuanza Januari mosi mwakani, ni karibu mara tatu ya bei ya sasa ambayo uniti moja hadi 50 huuzwa kwa Sh 60 na endapo ombi hilo litakubaliwa itauzwa kwa Sh 153.

Kwa ombi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, amewaomba wananchi na wadau wa sekta ya nishati kutoa maoni yao kupitia mkutano wa wazi utakaofanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam Desemba 2 saa nne asubuhi.

“Pia kwa wadau na wananchi watakaowasilisha kwa maandishi, watume kwetu wakati wowote kuanzia sasa hadi kabla ya saa 11 jioni Novemba 30,” ilieleza taarifa hiyo ya Masebu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ewura imeanza mchakato wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu uhalali wa ombi hilo la Tanesco kutokana na mapendekezo ya shirika hilo kuwa bei hizo mpya zianze kutumika Januari mosi mwakani. Ombi hilo limesajiliwa kwa namba TR-E-11¬-012 kulingana na kifungu cha 19(2)(b) cha Sheria, Sura 414 ya Sheria za Tanzania.

Bei na aina ya matumizi vilivyoainishwa katika taarifa hiyo vilionesha kuwa kundi la matumizi madogo ya nyumbani (kaya) inayoanzia uniti 0 hadi 50kWh itauzwa Sh 153 kutoka Sh 60 kwa sasa na kuanzia uniti 50 kuendelea, zitauzwa Sh 497 kutoka Sh 195 za sasa.

Vipengele vingine ni matumizi ya kawaida ambapo bei kwa kila uniti (kVh) ni Sh 400 kutoka Sh 157 na gharama ya huduma kwa mwezi ni Sh 3,106 kutoka Sh 2,738.



Katika msongo mdogo, gharama ya huduma kwa mwezi ni Sh 25,875 kutoka Sh 10,146 na bei kwa uniti ni Sh 240 kutoka Sh 94 ya sasa, wakati mahitaji kwa kVA yatakuwa Sh 30,802 kutoka Sh 12,078.

Aidha, matumizi katika msongo mkubwa yatakuwa Sh 25,875 kutoka Sh 10,146 wakati bei mpya kwa kila uniti itakuwa Sh 212 kutoka Sh 84 ya sasa na mahitaji ni Sh 26,395 kutoka Sh 10,350 ya sasa.

Kwa upande wa ZECO, gharama ya huduma kwa mwezi imependekezwa kuwa Sh 25,875 kutoka Sh 10,146 na bei ya kila uniti kuwa Sh 212 kutoka Sh 83 huku mahitaji kwa kVA yamependekezwa kuwa Sh 21,957 kutoka Sh 8,610 ya sasa.

Mkuu wa Mawasiliano ya Umma wa Ewura, Titus Kaguo, akizungumza na gazeti hili kuhusu suala hilo jana, alisema ombi hilo ni la dharura na limeletwa kutokana na ongezeko la gharama na miradi ya Tanesco, hivyo ni lazima wadau wapate nafasi ya kutoa maoni kabla ya kupitishwa.

Masebu katika taarifa yake, alisema Tanesco ilitoa ombi hilo kutokana na hali ya mvua mwaka 2010 na 2011 katika maeneo ya mabwawa iliyosababisha kuathiri uzalishaji na kuleta upungufu mkubwa wa umeme ulioathiri hali ya kifedha ya shirika hilo na uchumi kwa ujumla.

Alifafanua: “Ili kulimaliza tatizo hili, Tanesco ilisaini mikataba mitatu, mkataba na IPTL kuzalisha megawati 100 kwa kutumia mafuta mazito (HFO), wa kuuziana umeme (PPA) na Symbion LLC kuzalisha megawati 112 kutumia gesi asilia na mafuta na mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na Aggreko kuzalisha megawati 100 kutumia mafuta ya dizeli,”

Aliongeza: “Vilevile, Tanesco inatekeleza mradi wake wa megawati 150 ambao utatumia gesi asilia pamoja na mafuta na mradi mwingine wa megawati 70 ambao utatumia mafuta mazito (HFO), mbali na miradi itakayokamilika mwakani, umeme unaozalishwa kupitia mikataba hiyo umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la mgawo.

Lakini alisema juhudi za kumaliza tatizo hilo zimeongeza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji za Tanesco, suala lililofanya shirika hilo litoe ombi la dharura la kuongeza asilimia 155 ili kulipia gharama hizo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo mara baada ya kukusanya maoni ya wadau na kukamilisha mchakato wa kupitia ombi hilo la dharura, uamuzi utatolewa kupitia Agizo la Muda
.