Waokozi wanajaribu kuwaokoa manusura waliokwama katika vifusi vya majengo baada ya tetemeko la ardhi la kipimo cha 5.7 kukumba mji wa Van, kaskazini mwa nchi ya Uturuki.

Majengo kadhaa yameporomoka wakati tetemeko hilo liligonga, ikiwemo hoteli moja la ghorafa sita.

Takriban wafanyakazi 100 wa kutoa misaada na waandishi wa habari wanaaminika walikuwa wanaishi katika hoteli hiyo.

Waandishi hao walikuwa katika eneo hilo kwa sababu ya tetemeko lingine lililokumba eneo hilo wiki mbili zilizopita, ambapo watu wasiopungua 500 walikufa.


Baadhi ya waandishi waliokwama wamekuwa wakituma ujumbe mfupi wa simu ya mkononi wakiomba usaidizi.

Akizungumza  mbunge wa Uturuki, Nasmi Guhr, amasema '' Takriban majengo mengine 40 yameporomoka mjini Van na makundi ya waokozi wanajaribu kuokoa waliokwama''.

Picha za Televisheni kutoka Van zinaonyesha wakazi na waokozi wakijaribu kuinua vifusi ili kuwaondoa watu waliokwama katika majengo yaliyoporomoka.

Baadhi ya waandishi wa habari waliokwama katika majengo hayo wametuma ujumbe kupitia simu zao za mkononi wakiomba waokolewe.

Naibu wa Waziri Mkuu, Besir Atalay, amesema kuwa tetemeko hilo liliporomosha shule moja, nyumba kadhaa za udongo pamoja na hoteli.