Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imeonya kumchukulia hatua kali kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi kwa kujitangaza kuwa yeye ndiye Rais mpya wa taifa hilo.
Bwana Etienne Tshisekedi amejitokeza tena jana Jumapili na kutoa wito kwa Idara zote za serikali kumtii na kutaka vyombo vya usalama kutoitii tena serikali ya Joseph Kabila.Akihutubia mkutano wa waandishi wa habari mjini Kinshasa Jumapili, Tshisekedi alisema: "Naamuru maafisa wote wa jeshi na polisi kutii utawala wa kweli uliochaguliwa na Congo. Waache kutii watu ambao kesho watajieleza kwa mahakama za kitaifa na kimataifa kwa makosa waliyofanya wakati wa kutawala taifa hili."
Bwana Tshisekedi alitangazwa kuwa wa pili katika uchaguzi wa Urais akimfuatia Rais Joseph Kabila. Mahakama ya juu nchini humo pia ilithibitisha kuwa Rais Kabila ndiye aliyeshinda uchaguzi huo.
Tangu kampeni za uchaguzi wa Urais kuanza miezi miwili iliyopita na kisha kura kupigwa na kutangazwa na tume ya uchaguzi Tshisekedi amejitangaza mara tatu sasa kuwa ndiye Rais.
0 Comments