Vaclav Havel, mwandishi wa tamthilia aliyekuja kuwa rais wa kwanza wa Czechoslovakia, baada ya ukoministi, amefariki.
Alikuwa na umri wa miaka 75.
Rais huyo wa zamani amekuwa akiugua kwa miaka kadha, na mwaka wake wa mwisho, amekuwa akipumzika kwenye nyumba yake ya shamba.
Mwaka wa 1989 Vaclav Havel alikuwa mwandishi wa tamthilia aliyezungumza kwa upole, ambaye alifungwa kwa sababu ya msimamo wake wa kutetea demokrasia na sheria.
Alikuwa hajulikani na wengi, lakini katika majuma machache waandamanaji waliokusanyika kupinga ukoministi walianza kutaja jina lake kwa kelele.
Na Disemba mwaka wa 1989, jambo ambalo hata halikufikiria lilitokea - mwandishi huyo akawa rais wa Czechoslovakia.
Miaka mitatu baadae alishuhudia nchi yake ikigawika pande mbili - Czech na Slovakia - jambo ambalo hajakubaliana nalo, na lilimuumiza sana.
Lakini aligombea urais tena katika Jamhuri ya Czech huru, na aliongoza nchi hadi mwaka 2003.
Baada ya kustaafu alikuwa akitunga tamthilia, na mwaka jana alifanikiwa kupata ndoto yake..kwa kuwa mkurugenzi (director) wa tamthilia yake ya karibuni kabisa. BBC
0 Comments