KUTOKA GAZETI LA NIPASHE.

Baadhi ya wasomi wa vyuo vikuu vilivyopo mjini hapa wameitaka serikali kuacha mara moja tabia ya kurundikiana vyeo wakati kuna wasomi wengi ambao hawana ajira.
Kauli hiyo waliitoa mwishoni mwa wiki wakati wa mafunzo yaliyoendeshwa na uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Dodoma uliofanyika kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanavyuo na wanafunzi wa shule za sekondari juu ya sababu za kupinga sheria ya mchakato wa kuandika katiba mpya.
Wasomi walidai inasikitisha kuona viongozi wa serikali ambayo inaongozwa na CCM imekuwa ikijilimbikizia vyeo jambo ambalo linasababisha vijana wengi kukosa ajira.
Wakizungumzia juu ya vyeo vya wakuu wa mikoa na wabunge, walisema hakuna sababu yoyote ya rais kuwateua wabunge kuwa wakuu wa mikoa wala wakuu wa wilaya na badala yake kila mtu awe na nafasi ya kazi ili kuepusha msongamano wa ukosefu wa ajira.
Kwa upande wake, mwendesha semina hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo taifa, Chadema, Benson Kigaira, aliwataka wanavyuo kutoa elimu kwa jamii juu ya kushiriki kupinga kuendelea kwa mchakato wa katiba mpya.
Alisema pamoja na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, kukataa kuwasilikiza viongozi wa Chadema, kinachofanywa ni kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi hususani vijijini.
Aliwataka wanaChadema na wananchi kwa ujumla wasikubaliane na uandikwaji wa katiba mpya kwa sababu itakuwa ni ya kutetea maslahi ya viongozi na wanachama wa chama wa CCM.
Alisema kwa sasa viongozi wa Chadema wamejipanga kuhakikisha wanatoa elimu kila mahali hususani vijijini ili kuwaondoa wasiwasi wale ambao wanadai kuwa Chadema ni chama cha fujo.