WANANCHI wa Kenya wamepongeza maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara
ambayo imefunikwa na amani na utulivu sifa iliyodumu mpaka leo baada ya kupata Uhuru 1961 kutoka kwa wakoloni.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari mkoani Mara kwa niaba ya wananchi wa nchi hiyo, Ofisa Wilaya ya Kuria Magharibi Tarafa ya Isibania, nchini Kenya, Thuo wa Ngugi, ambaye alikuwa kati ya wageni waalikwa katika sherehe za Uhuru mjini hapa jana alisema kuwa utulivu uliooneshwa na Watanzania ni wa kuigwa duniani na Watanzania.
“Kitu cha kujivunia kwa Watanzania ni amani na utulivu walionao pia wasiruhusu mtu au chama chochote cha siasa kuvunja amani hiyo hata sisi wa Kenya tunaililia amani hii,” alisema Ngugi.
Alisema kuwa nchi ya Tanzania imejipatia mafanikio mengi ambayo awali wakati wa ukoloni hayakuwepo kwani wakoloni walitumia muda huo kuwanyonya na kuhamisha raslimali za Afrika kupeleka nchini kwao.
“Tunawapongeza Watanzania kwa hili kufikisha miaka 50 ya Uhuru bila vita na machafuko ya ndani si mchezo kwani watu wengi wanalilia amani hii ya Watanzania hasa nchi zote za ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla hata baadhi ya nchi za mabara mengine,” alisema.
Ngugi alikuwa mmoja wa wageni waalikwa kutoka katika nchi ya Kenya ambaye alihudhuria katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru yaliyofanyika kimkoa Manispaa ya Musoma.
0 Comments