Diwani wa Kata ya Kibaigwa, Richard Kapinye, akiwasihi wakulima wa mashamba makubwa waliondolewa wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara kutoandamana katika mji wa Kibaigwa, mkoani Dodoma jana, wakipinga kuhamishwa katika vijiji vyao.

MAANDAMANO YA WAKULIMA
Wakulima wa matrekta wasafiri masafa marefu kulalamika
  
Singida ni mshikemshike kati ya Polisi, wafanyabiashara
Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma, limezima maandamano ya wakulima wakubwa kutoka vijiji tisa vya wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara, wameandamana wakiwa na matrekta takribani 200 kupinga kuondolewa katika mashamba yao ili kupisha hifadhi za mbuga za wanyama.
Wanaotakiwa kupisha mbuga za wanyama ni wakulima wa mashamba makubwa kutoka vijiji vya Lendolai, Mlimahamba, Laitini, Mbigiri, Kutilemeinyi, Seseni, Laipela, Kimarai na Kisima.
Tukio hilo lilitokea jana katika mji mdogo wa Kibaigwa, ambapo ilimlazimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Stephen Zelothe, kutuma ujumbe kwa wakulima hao akiwataka kutoandamana na badala yake kuegesha matrekta yao pembeni mwa barabara ya kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Lakini wakati wakiwasubiri viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwenda kuwasikiliza, baadhi ya wakulima hao waliingia barabarani na kuzuia magari yaliyokuwa yakiitumia barabara hiyo kwa muda, kabla ya kukubali kuondoka, baada ya Diwani wa Kata ya Kibaigwa, Richard Kapinye, kuwasihi waondoke njiani.

“Nawaomba muondoke barabarani jamani, tumeahidiana kuwa tutawasubiri viongozi waje wazungumze nasi na kutoa majibu, sasa mkifanya hivi watashindwa kusaidia,” alisema Kapinye kwa kutumia gari lililokuwa na kipaza sauti.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima hao, walisema walianza kulima katika mashamba hayo mwaka 1990, baada ya kupewa na wenyeji.
Mmoja wa wakulima hao, Clement Petro, alisema ilipofika mwaka 2006, walikwenda watu kutoka serikalini na kuwaambia waondoke katika eneo hilo ili kupisha hifadhi ya mbuga.
Alisema walipeleka kesi mahakamani ambapo mahakama iliwapa ushindi wa kuendelea na shughuli zao katika eneo hilo.
Hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto ilikata rufaa kupinga hukumu hiyo ambapo ilishinda na wakulima hao wakaamuliwa kuondoka katika eneo hilo.
Mkulima mwingine, Omary Athuman, ambaye anamiliki matrekta wilayani humo, alisema kutokana halmashauri hiyo kuwafukuza katika eneo hilo, ana wasiwasi kama ataweza kurejesha mkopo wa matrekta aliyokopa kutoka Shirika la Uchumi la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) tawi la Dodoma.
“Tumeamua kuja huku kwa kuwa eneo la Kiteto halina amani tena kwa sababu wafugaji wamekuwa wakipitisha mifugo katika mashamba yetu wakidai kuwa tumeshaambiwa tuondoke katika eneo hilo,” alisema.
Alisema pia wameamua kufanya maandamano hayo na kueleza kilio chao kwa kuwa wamekuwa wakiuza mazao yao katika soko la Kibaigwa na pia mkopo wa matrekta wameupata kutoka Suma JKT mkoani hapa.
“Mimi sijui hii dhana ya Kilimo Kwanza inatekelezwaje, mwanzoni tulidhani ni sera nzuri, lakini hivi sasa tunadhani haitekelezwi kivitendo na sijui haya matrekta tutalipa kwa fedha kutoka wapi,” alisema na kuongeza kuwa yeye ana ekari 300 ambazo analima mahindi.
Kwa upande wake, Alli Khalifan Said, alisema kuwa tayari wameandaa mashamba kwa ajili ya kilimo hivyo kuamriwa kuondoka katika eneo hilo itakuwa ni hasara kubwa kwake.
“Wanataka tuondoke katika eneo hili, lakini hawatuambii twende wapi wala nani atalipia matrekta tuliyokopa na nyumba tulizojenga,” alisema Said.
Wakulima hao waliomba viongozi wa ngazi za juu, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, kuingilia kati suala hilo ili waweze kurudishiwa ardhi hiyo na kuendelea na uzalishaji.
KAULI YA DED KONGWA
Akizungumza na wakulima hao, Mkurugenzi Mtendaji (DED) wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Athuman Akalama, alithibitisha kupokea barua ya kuomba kusaidiwa kutoka kwa wakulima hao.
Hata hivyo, alisema wilaya za Kiteto na Kongwa ni wilaya mbili tofauti ambazo kila moja ina utaratibu wake wa matumizi bora ya ardhi.
“Ni kama vijiji vinapokuwa na utaratibu wake wa matumizi bora ya ardhi. Mimi siwezi kufahamu ardhi hiyo walipanga kwa ajili ya matumizi yapi,” alisema.
Alisema nchi imekuwa ikiendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria na kuwashauri wakulima hao kwenda kukata rufaa mahakamani kudai haki zao kwa kuwa kuandamana na kupanga matrekta mahali hapo hakutawasaidia kutatua tatizo hilo.
WAKULIMA WAZOMEA
Baada ya kumaliza kuzungumza na kuwahoji kama wamekubaliana, kundi la wakulima lilizomea.
Hata hivyo, wakulima hao walikubali kutoka katika eneo hilo huku Akalama aliyeongozana na viongozi wengine wa wilaya hiyo wakiondoka chini ya ulinzi wa polisi katika eneo hilo.
SOKO LA KIBAIGWA LATIKISWA
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Soko la Kibaigwa, Kusekwa Dalali, alisema wamekuwa wakipokea mazao katika baadhi ya maeneo kutoka katika mikoa mitano ambayo ni Dodoma, Morogoro, Manyara, Iringa na Tanga.
Alisema mazao ambayo wanayapokea katika soko hilo ni mahindi, alizeti, mbaazi, tetere, nyonyo na maharage na kwamba asilimia 60 ya mazao hayo yanatoka wilayani Kiteto, mkoani Manyara.
“Kama wakulima wamezuiwa kulima katika maeneo hayo, sielewi itakuaje kwa sababu asilimia 60 ya mazao inatoka wilayani Kiteto,” alisema na kuongeza kuwa katika msimu wa mavuno wamekuwa wakipokea tani 1,000 kwa siku.
Alisema kutokana uamuzi huo wa serikali, soko hilo la kimataifa la mazao ya nafaka nchini, lililojengwa na Muungano wa Vikundi vya Wakulima nchini (Mviwata) na Ufaransa, huenda likashindwa kufanya kazi.
POLISI, WAFANYABISHARA WAPAMBANA SINGIDA
Wakati huo huo, mtarafaruku mkubwa umeibuka kati ya wafanyabiashara wa kuku na uongozi wa Manispaa ya Singida, hali iliyotishia uvunjifu wa amani na polisi kuingilia kati na kuwatia mbaroni watu kumi.
Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 10:00 jioni, muda mfupi baada ya wajasiriamali hao kupakia kwenye lori matenga 27 yenye kuku, tayari kwa ajili ya kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, baadaye lori hilo aina ya Fuso lenye namba za usajili T. 125 BES, lilikamatwa na askari wa usalama barabarani waliokuwa na watumishi wa manispaa wakati likiwa nje ya mji katika barabara kuu ya Singida-Dodoma. Baada ya lori hilo kurudishwa mjini, na kushikiliwa katika ofisi za manispaa, kundi la wafanyabiashara wa kuku lilivamia eneo hilo na askari mmoja wa kikosi cha usalama barabarani alichaniwa sare yake ya shati.
Kutokana na vurugu hizo kuwa kubwa, Jeshi la Polisi lilipeleka askari wengi katika ofisi za Manispaa ya Singida kwa ajili ya kudhibiti vurugu hizo na kuleta utulivu na kuwatia mbaroni wafanyabiashara kumi wa kuku.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Cordula Lyimo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, ingawa hakuwa tayari kutaja jina la askari aliyechaniwa sare wala wanaoshikiliwa kwenye vurugu hizo, kwa maelezo kuwa hakuwa amepata taarifa rasmi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Chama Cha Wauza Kuku Mjini Singida, Selemani Kuku, Mwenyekiti wa chama hicho, Karani Mahiki na Katibu wake, Msafiri Juma, ni miongoni mwa watu waliokuwa wanashikiliwa na jeshi hilo tangu juzi jioni. Kuku alifafanua kuwa pia wapo wafanyabiashara wengine sita ambao pia walikuwa wanashikiliwa, huku dereva wa lori hilo aliyetajwa kwa jina moja la Masawe, akiachiwa huru.
Kwa muda mrefu, wafanyabiashara hao wamekuwa wakipinga kitendo cha manispaa kuongeza ada ya ushuru hadi kufikia Sh. 12,000 kwa tenga moja lenye uwezo wa kuchukua kuku 80, au kuku mmoja kulipiwa ushuru wa Sh. 300, ikilinganishwa na awali ambapo tenga moja lilipiwa Sh. 1,000.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Salome Singano, alisema kuwa ada hizo mpya zimetokana na maamuzi ya kikao cha Baraza la Madiwani cha Aprili, mwaka huu, kisha kusainiwa na Waziri Mkuu, kabla ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Oktoba7, 2011.
Singano, alisema mchakato wa sheria hiyo inayojulikana kama ’Sheria ndogo ya Halmashauri ya Manispaa ya Singida, ada na ushuru 2011’, ilipelekwa kwanza kwa wananchi na kubandikwa katika mbao za matangazo kabla ya kurudishwa katika Baraza la Madiwani na baadaye kwa Waziri Mkuu.