TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nape Nnauye
Hivi karibuni kumeibuka mjadala juu ya ongezeko la posho za wabunge kwa karibu ya asilimia 200, kutoka sh. 70,000 hadi sh. 200,000.

Malipo hayo yaliyoibua mjadala baina ya wadau mbalimbali, ni yale yanayohusisha posho ya kikao cha bunge kwa siku.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefuatilia kwa makini suala hilo la nyongeza ya posho hiyo ya wabunge kama lilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na baadae kutolewa maelezo na Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashilila na Spika wa Bunge Anne Makinda.

Kwa namna suala lenyewe linavyopewa msukumo, CCM imeona si vema kukaa kulikalia kimya na hivyo imetoa msimamo wake kama ifuatavyo:-

i. Linapotekelezwa jambo lolote kwa kigezo cha ugumu wa maisha au kupanda kwa gharama za maisha, ni lazima jambo husika lilenge kutatua ugumu huo wa maisha kwa makundi yote katika jamii na si kwa makundi machache ndani ya jamii.

ii. Kwa kuongeza kiwango hicho cha posho kwa wabunge ni kuongeza pengo/tofauti ya mapato kati ya wenye nacho na wasionacho katika jamii yetu hasa kwa kuegemea baadhi ya makundi.

iii. Bunge ni chombo muhimu cha kutunga sheria, kinapoibuka na madai kwamba sababu za kuongezeka kwa posho hizo kunatokana na kupanda kwa gharama za maisha mjini Dodoma kama alivyoainisha Spika wa Bunge, ndiyo inasababishahofu na mashaka miongoni mwa Watanzania. Na kwa kweli swali kubwa kwa Watanzania hao ni je, maisha yanapanda Dodoma pekeake na kwa wabunge tu?

Hivyo basi CCM inashauri kwa kuzingatia masilahi mapana ya nchi na jamii yetu kwa ujumla, waheshimiwa wabunge wetu na mamlaka zingine zinazohusika na swala hili, kulitafakari upya jambo hili.

Tunaamini busara itatumika kuachana na jambo hili, kwani kuendelea nalo kunaweza kutafisiriwa ni kuwasaliti watendaji katika sekta nyingine wakiwemo Walimu, askari, Madaktari na wengineo.

Ni muhimu ifahamike kuwa kuongoza ni kuonesha njia, hivyo si sahihi kwa wabunge kuonesha njia kwa kujiongezea posho peke yao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha huku wakiwaacha wananchi ambao ndiyo wanaowawakilisha bungeni wakikosa nafasi ya kupunguza ugumu wa maisha unaowakabili, jambo ambalo ni hatari.

Katika hatua nyingine, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinawapongeza sana Watanzania kwa ujumnla wao, bila kujali tofauti zao za kiitikadi, kwa kushiriki kwa amani na utulivu katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Ushiriki wao kwa pamoja, umeyafanya maadhimisho hayo yafane sana. CCM inaamini kuwa maadhimisho haya ya miaka 50 yatatumika kuendelea kujenga uzalendo, umoja na mshikamano wan chi yetu katika kufikia maendeleo.

Imetolewa na:-Nape M. Nnauye,KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFAITIKADI NA UENEZI11/12/2011