MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Dodoma jana ilimhukumu kifungo cha miaka 30 jela mhudumu wa usafi wa Msikiti wa Masjid Ghazal, Bashiri Hassan (36), baada ya kukiri mashitaka ya kumlawiti mvulana wa miaka 11 katika choo cha Msikiti huo.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Adrian Kilimi, baada ya kumtia hatiani mshitakiwa kutokana na kukiri mashitaka.
Kabla ya adhabu hiyo kutolewa, Wakili wa Serikali Godfrey Wambali aliomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa kwa kuwa kosa alilofanya ni la kufedhehesha jamii na halifai katika maisha ya binadamu.
Alipopewa fursa ya kujitetea, mshitakiwa alidai hana la kusema na yote anamuachia Mungu ili amtetee; “Namwachia Mungu ili anitetee.”
Akitoa adhabu hiyo Hakimu Kilimi alisema kitendo alichofanya mshtakiwa ni kibaya lakini hata hivyo hakuisumbua Mahakama kuingia gharama kuendesha kesi hiyo na kuepusha muda wa Mahakama kupotea.
Alisema kwa kuwa mshitakiwa amekiri mashitaka, Mahakama inampa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Awali, ilidaiwa kuwa mshitakiwa ambaye ni mkazi wa Bahi Road, alimlawiti mvulana mwenye umri wa miaka 11 baada ya kumuingiza kwenye choo cha Msikiti huo upande wa wanawake.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Januari 23, mwaka huu majira ya jioni. mwisho
0 Comments