Zacharia Osanga
"Ee Mungu tunaiombea timu yetu (Taifa Stars) ifanye vizuri katika medani za kimataifa na ifuzu katika mechi mashindano ya kimataifa na kufikia hatua ya kucheza Kombe la Dunia Brazil mwaka 2014.

"Baba tunakuomba uibariki timu yetu...Baba tunakuomba uipe mafanikio, ifanye vizuri icheze Kombe la Dunia...," ni kauli ya Askofu Charles Gadi wa Huduma ya Good News for All wakati akiiombea Taifa Stars jana.

Gadi alifanya hivyo wakati wa maombi 1,000 ya kuliombea Taifa la Tanzania katika Jubilei ya miaka 50 ya Uhuru yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Biafra, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Lakini kabla ya kufanya maombi hayo, Askofu Gadi alisema klabu za Tanzania zinashindwa kupiga hatua za mbali katika medani ya soka katika ngazi mbalimbali kutokana na kuweka mbele uchawi badala ya kucheza soka kisayansi na kumuomba Mungu.

"Soka ya Tanzania iko chini...kiwango cha soka katika nchi yetu hakikui kutokana na klabu nyingi kutegemea ndumba kama nyenzo ya mafanikio badala ya kumtegemea Mungu.

"Ushindi hauji kwa ndumba, ushindi hauji bila kumuomba Mungu, tubadilike tuachane na ndumba ili kupata mafanikio...," alisema.

Gadi alisema kuwa anafanya maombi hayo, dhumuni hasa ni kuona Taifa Stars inafuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil mwaka 2014.



Alisema kuwa tendo wanalolifanya ni la kiimani zaidi na picha waliyotumia yenye wachezaji wa Taifa Stars, pamoja na mpira viliombewa kwa niaba ya timu hiyo.

Mbali na maombi hayo ya Taifa Stars na soka ya Tanzania, pia kulifanyika maombi ya kuliombea taifa baada ya kutimiza miaka 50 ya uhuru, ili kuondoka na laana ambazo zimesababisha nchi kutokuwa na mafanikio katika sekta mbalimbali ikiwemo hiyo ya michezo licha ya kuwa na raslimali nyingi kama mito, maziwa na bahari.

Askofu huyo alisema kuwa maombi hayo yameanza jana na yatachukua miaka mitatu na yatakuwa yakifanyika katika makanisa mbalimbali kila siku.

Tangu Uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961, Taifa Stars imefanikiwa kushiriki Fainali za Afrika moja tu za Afrika mwaka 1980, na kufanya vibaya fainali hizo, na tangu hapo haijawahi kukata tiketi hiyo.

Wakati maombi yakifanyika kuipeleka Taifa Stars Brazil, timu hiyo haijawahi kufanya vizuri na ina kazi ngumu ya kufuzu kwani iliitoa kwa mbinde timu dhaifu ya Chad baada ya kuilaza mabao 2-1 mjini N'Djamena kabla ya kulizwa bao 1-0 jijini Dar es Salaam mechi ya marudiano hivyo kupenya kwa mabao ya ugenini.

Kutokana na hatua hiyo, Stars imepangwa Kundi C la michuano hiyo pamoja na Ivory Coast, Gambia na Morocco. Timu itakayoongoza ndiyo itakayokata tiketi ya Brazil. Mechi zitaanza kuchezwa Juni mwaka huu.