Awapiga marufuku kukusanyika
Awataka warudi kazini au wafukuzwe
Wenyewe wasema wanaenda mahakamani
Serikali imewageuzia kibao madaktari walioko kwenye mgomo baada ya kuwataka kuacha mara moja mgomo huo na kuripoti kazini leo na kuonya kuwa yeyote atakayeshindwa kufanya hivyo atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.

Pia imeviagiza vyombo vya dola kuwashughulikia madaktari wote watakaofanya mkutano mahali popote kujadili mgogoro wa maslahi yao kwa vile mikutano hiyo ni kinyume cha sheria.
Vile vile, imeiagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kupeleka madaktari wake katika hospitali za mkoa wa Dar es Salaam ili kusaidia wagonjwa walioko hospitalini, ambako imesema huduma zitaendelea kama kawaida.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, jana alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, baada ya madaktari hao kukataa kukutana naye ili kupata suluhu ya mgogoro huo.
Juzi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka, alithibitisha kupokea wito wa Waziri Mkuu wa kukutana na madaktari jana, lakini akasema ulichelewa kuwafikia.
Alisema kutokana na hali hiyo wasingekuwa tayari kukutana naye jana, badala yake wangekutana leo na baadaye kufanya mikutano ya hadhara katika tarehe na mahali ambako wangepatangaza baadaye.


“Kuanzia sasa serikali inawahimiza madaktari wote walio katika mgomo kuacha mara moja na kuripoti kazini ifikapo kesho (leo) asubuhi, Jumatatu tarehe 30 Januari, 2012. watakaoshindwa kufanya hivyo, watakuwa wamepoteza ajira zao,” alisema Pinda.
Aliongeza: “Mikutano (ya madaktari walioko kwenye mgomo) inayofanyika ni kinyume cha sheria. Hivyo, naviagiza vyombo vya dola tusiiruhusu. Hakuna (kukutana) Starlight, Don Bosco wala wapi,” alisema Pinda.
Mkutano huo wa jana ulihudhuriwa na mawaziri, Dk. Haji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), George Mkuchika (Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi), Shamsi Vuai Nahodha (Mambo ya Ndani ya Nchi), Dk. Hussein Mwinyi (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa-JKT), Dk. Lucy Nkya (Naibu Waziri-Afya na Ustawi wa Jamii) na Hawa Ghasia (Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma).
Wengine waliohudhuria ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime pamoja na maofisa wa wizara hiyo.
Alisema mgomo unaofanywa na madaktari hao siyo halali kwa vile haukufuata taratibu za kuitisha mgomo.
Pinda alisema madaktari walipaswa kutangaza mgogoro na kisha kutoa notisi ya siku 60, jambo ambalo alisema hawakulifanya.
Alisema katika muda huo wa notisi wa siku 60, majadiliano yalitakiwa yawe yanaendelea ili kushughulikia madai yao.
“Nawaomba sana mgomo ukome, tuache, maana ukiendelea watu wataumia. Tukiwaita kwenye vikao hawaji. Mwisho tutaonekana hatuna heshima. Kwa hiyo, kesho warudi kazini kama kawaida. Atakayeshindwa tutamhesabu si mtumishi,” alisema Pinda.
Alisema kwa uamuzi huo anajua serikali itapata changamoto, lakini akasema ni bora waendelee na changamoto hiyo kuliko iliyopo sasa ya wagonjwa kuendelea kuumia.
Kutokana na hilo, aliitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuandaa utaratibu wa kuwarudisha kazini madaktari wote walioko kwenye mgomo.
Pia aliwataka wakuu wa mikoa na hopsitali zote kufuatilia kwa karibu zaidi kuona madaktari walioko kwenye mgomo kama wataendelea kutoa huduma leo.
Alisema katika hatua iliyofikiwa, serikali imetambua kwamba madaktari wanaoongozwa na Kamati ya Mpito, hawataki suluhu licha ya juhudi zote ambazo zimefanywa za kuwaita ili kushughulikia madai yao.
Waziri Mkuu alisema serikali imebaini pia kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Stephen Ulimboka siyo mtumishi wa serikali na wala hajasajiliwa kama daktari.
KUHUSU DK. ULIMBOKA
Pinda alisema Dk. Ulimboka alihitimu Shahada ya Udaktari (MD) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2004, alipata usajili wa muda wa Baraza la Madaktari mwaka huo huo na kupangiwa internship katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Alisema Novemba 2005 aliongoza mgomo wa madaktari nchini na usajili wake ulisitishwa na Baraza hilo.
Pinda alisema alishtakiwa mbele ya baraza hilo kwa ukiukwaji wa maadili ya taaluma ya udaktari kwa kuitisha na kufanya mgomo ambayo ni makosa ya kimaadili katika taaluma hiyo.
Alikataa kufika mbele ya baraza kujibu tuhuma zilizokuwa zinamkabili na hivyo, shauri lake halikumalizika.
Alisema Julai 2006, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alimsamehe na hivyo kurejeshewa usajili na baraza na kuruhusiwa kuendelea na internship.
Pinda alisema katika kumpa taarifa za msamaha wa Rais, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Baraza la Madaktari kwa nyakati tofauti walimtaka Dk. Ulimboka kutojihusisha na mgomo au suala lolote ambalo ni kinyume cha maadili ya taaluma ya udaktari.
Alisema Dk. Ulimboka kupitia barua yake kwa baraza ya Februari 2, 2007, alikiri kwamba hatajihusisha wala kutoa ushawishi wowote kwa wengine kufanya vitendo ambavyo ni kinyume cha maadili ya udaktari.
“Hadi sasa hakuna taarifa kama alimaliza internship kwa kuwa hajawasilisha cheti cha kumaliza mazoezi hayo na hakuna taarifa juu ya mahali anapofanyia kazi. Aidha, Dk. Ulimboka siyo mtumishi wa serikali na wala hajasajiliwa kama daktari,” alisema Pinda.
MADAI YA MADAKTARI
Waziri Mkuu alisema kulikuwa na mawasiliano kati ya ofisi ya Waziri Mkuu na uongozi wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) na baadaye mwenyekiti wa muda wa kamati ya mpato ya madaktari kuhusu mgomo wa madaktari.
Alisema katika barua yao ya Januari 27, mwaka huu, walitoa madai manane; ikiwamo posho ya kulala kazini, posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi, posho ya nyumba, posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu, kupatiwa posho ya usafiri, nyongeza ya mshahara, kupatiwa huduma ya bima ya afya na kutaka wenzao warudishwe Muhimbili.
Pinda alisema madaktari hao wanadai mshahara wa Sh. 700,000 kwa daktari anayeanza kazi ni mdogo sana, hivyo wanapendekeza alipwe Sh. milioni 3.5 kwa mwezi.
Alisema wakati madaktari hao wakipendekeza kwamba madaktari wanaoajiriwa hivi sasa walipwe kiasi hicho cha mshahara, madaktari wapya wanaoajiriwa wanalipwa Sh. 957,700 wakati watumishi wa kada nyingine kama wahandisi wanaanza na Sh. 600,000, wahasibu kati ya Sh. 300,000 hadi 400,000.
Pinda alisema posho zote wanazodai madaktari zikijumuishwa zinafikia asilimia 120 ya mshahara wa daktari mmoja.
Alisema ili kuhakikisha kunakuwa na hali ya utulivu katika mazingira ya kazi, utekelezaji wa pendekezo la madaktari la kulipa mshahara wa Sh. milioni 3.5, kwa mwezi kwa daktari atakayeanza kazi, utailazimu serikali kurekebisha viwango vya mishahara kwa watumishi wote wa kada za afya pamoja na kada nyingine ili kuweka uwiano kufuatana na stahiki za miundo katika utumishi wa umma.
Pinda alisema kwa mujibu wa mapendezo yao, ina maana kwamba kiwango cha kuanzia mshahara kwa mhudumu wa afya kitakuwa Sh. 670,316 na mshahara wa juu kwa kada za afya utakuwa Sh. 8,145,573 kwa mwezi.
Alisema utekelezaji wa pendekezo hili utagharimu jumla ya Sh. 83,508,834,430 kwa mwezi ambayo ni sawa na Sh. 417,544,172,150 kwa kipindi kilichobaki cha miezi mitano na kwamba, kiasi hicho ni sawa na nyongeza ya Sh. 301,730,372,400 katika bajeti ya mshahara kwa mwaka 2011/2012.
Pinda alisema kwa mujibu wa mapendekezo ya madaktari ya mshahara pamoja na posho mbalimbali itamaanisha daktari anayeanza kazi atapata jumla ya Sh. milioni 7.7 kwa mwezi ikijumuisha mshahara na posho nyingine.
Alisema pia kwa mujibu wa mapendekezo hayo, daktari mshauri mwandamizi atapata Sh. 17,231,020 kwa mwezi na kwamba, kwa kuzingatia ukubwa wa gharama hizo utekelezaji wa mapendekezo ya madaktari utakuwa hauwezekani kwa kuzingatia hali halisi ya bajeti ya serikali.
Alisema endapo serikali itatekeleza madai yao kwa mwaka mmoja, jumla ya mishahara yao itakuwa ni Sh 799,692,615,592 badala ya Sh. 222,214,936,800 za sasa hadi kufikia Juni, mwaka huu.
Waziri Mkuu alisema madaktari hao wanadai kwamba watumishi wa kada nyingine za afya wapandishiwe mishahara na posho kama zao na kwamba, endapo watapewa fedha wanazodai, serikali itapaswa kulipa Sh. 202,413,397,568 na kama madai yao yatatimizwa kwa miezi mitano iliyobaki, watapaswa kulipwa Sh. 84,338,915,653.
Alisema katika makundi hayo mawili tu, nyongeza yao ya mishahara ni sawa na Sh. 1,002,106,013,160 kwa mwaka.
Pinda alisema ukijumuisha na nyongeza ya posho zao wanazodai za Sh. 1,037,184,854,550 unapata Sh. 2,039,290,867,710, ambayo ni sawa na theluthi mbili ya mishahara ya wafanyakazi wote serikalini ambayo kwa sasa ni Sh. trilioni 3.45.
“Hii maana yake ni kwamba kiasi kinachobaki cha theluthi moja ndicho kigawanywe kwa watumishi wengine,” alisema Pinda.
MADAI YA KUTAKA WATENDAJI WAKUU WAJIUZULU
Pinda alisema madai mengine ya madaktari hao, wanataka Dk. Mponda, Naibu wake, Dk. Nkya, Katibu Mkuu, Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Mtasiwa wajiuzulu kwa madai ya kuzembea madai yao.
Hata hivyo, alisema iwapo hoja ni hiyo, hakuna anayeweza kubaki serikalini kwa vile wao ndio wako jikoni wanaona ugumu wa utekelezaji wa madai yao.
Alisema kumuondoa waziri kuna sababu zake na kuhoji: “Hivi nijiuzulu kwa sababu ya kusema ukweli? Nitakwambia sijiuzulu. Labda kama kuna jambo lingine.”
HALI ILIVYO KATIKA HOSPITALI
Waziri Mkuu alisema tangu mgomo uanze, serikali imekuwa ikifuatilia na kupokea taarifa za mgomo huo kutoka mikoa yote na kwamba, mpaka Januari 28, mwaka huu, mikoa 21 ilikuwa imewasilisha taarifa za awali juu ya hali ya mgomo huo.
Aliitaja mikoa ambayo hospitali zake zote za mikoa na wilaya hazina mgomo kabisa kuwa ni Ruvuma, Lindi, Mtwara, Shinyanga, Arusha, Tabora, Kagera, Iringa, Mara, Pwani, Kigoma, Singida, Manyara na Rukwa.
Aliitaja mikoa ambayo hospitali zake za mikoa (isipokuwa za wilaya) zimekuwa katika mgomo kuwa ni Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Morogoro, Tanga, Dodoma na Dar es Salaam, mbako ndiko ulikoanzia.