MWILI unapokosa kinga imara, huwa katika hatari ya kushambuliwa na kila aina ya magonjwa. Katika orodha hiyo ya magonjwa, yamo pia yale ya kutokwa uvimbe, yakiwemo majipu, kitaalamu yanajulikana kama ‘Inflamatory deseases’!.
Katika kukabiliana na matatizo kama hayo, nanasi ni moja kati ya matunda yenye vitamini nyingi na virutubisho vingine vyenye uwezo wa kutoa kinga kwenye mwili wako dhidi ya magonjwa hayo na mengine.
Siri na umuhimu wa nanasi, upo kwenye kirutubisho aina ya ‘Bromelain’ ambacho kinapatikana kwa wingi kwenye tunda hili na hivyo kulifanya kuwa tunda muhimu sana katika kujenga na kuimarisha kinga ya mwili.
Ukilipa umuhimu na ukiliweka nanasi katika orodha ya matunda unayokula mara kwa mara, utajiepusha na utajipa kinga dhidi ya magonjwa mengi, hususan ugonjwa wa kuwashwa na kuvimba koo, ugonjwa wa Baridi Yabisi (Arthritis) na ugonjwa gauti (Gout).
Ili upate kinga dhindi ya maradhi hayo kwa kula nanasi, unashauriwa kula nanasi kabla au baada ya kula mlo wako, usile nanasi pamoja na chakula kingine kwa wakati mmoja, kwa kufanya hivyo, virutubisho vitafanyakazi nyingine tofauti na uliyokusudia. Faida nyingine za nanasi ni kama ifuatvyo;

USAGAJI WA CHAKULA
Nanasi lina virutubisho vinavyouwezesha mfumo wa usagaji chakula tumboni kufanya kazi yake ipasavyo, pindi mfumo huu unapowezeshwa kufanyakazi yake vizuri, mtu huweza kupata choo laini na kwa wakati kama inavyotakiwa.

KINGA YA MWILI
Nanasi linaaminika pia kuwa miongoni mwa matunda yenye chanzo kizuri cha vitamin C ambayo kazi yake ni kuupa mwili kinga dhidi ya ‘wavamizi’ mbalimbali (free radicals), ambao wanapoingia mwilini, kazi yao hua ni kuharibu chembembe hai za mwili.
Kwa kuongezea, vitamini C inaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili, hivyo kuifanya kuwa kinga ya magonjwa madogo kama vile mafua, kikohozi, homa na maambukizi mengine.



CHANZO CHA MADINI
Mbali ya kuwa ni chanzo kizuri cha vitamin C, nanasi pia ni chanzo kizuri cha madini aina ya ‘manganese’ ambayo yanaaminika kuwa na uwezo wa kuboresha ufanisi wa vimeng’enyo mbalimbali vya mwili, vikiwemo vya kuzalisha nishati na kinga ya mwili. Halikadhalika tunda hili lina kiwango cha kutosha cha vitamin B1 (thiamin).

KUIMARISHA NURU YA MACHO
Inawezekana karoti ikawa ndiyo inayojulikana na watu wengi kuwa na uwezo wa kuimarisha nuru ya macho, lakini nanasi nalo lina uwezo mkubwa wa kuimarisha nuru ya macho. Utafiti unaonesha kuwa ulaji wa tunda hili na matunda mengine, kiasi cha milo mitatu kwa siku, kunaondoa hatari ya kupungua kwa nuru ya macho kwa asilimia 36 kwa watu wazima.

NANASI LILILO BORA
Nanasi lililo bora ni lile kubwa na lililoiva vizuri. Wakati ni kweli kwamba nanasi kubwa lina nyama nyingi kuliko nanasi dogo, lakini hakuna tofauti ya ubora wa virutubisho kati ya nanasi dogo na kubwa, ilimradi lisiwe limeoza au lenye michubuko mingi. Hivyo chagua nanasi lililoiva vizuri na lenye kunukia.
Mara baada ya nanasi kumenywa na kukatwa vipande, linatakiwa kuliwa mara moja, iwapo litahifadhiwa kwenye jokofu kwa ajili ya kuliwa baadaye, njia sahihi ya kuhifadhi ni kuliweka kwenye chombo chenye mfuniko (container) ili kuhifadhi virutubisho vyake kwa kipindi hadi cha siku tano bila kupoteza ubora wake, ikiwa pamoja na ladha. Unaweza kula vipande vya nanasi au juisi yake, kote kuna faida.

Toka Gpl.