Nora Damian
MKAZI wa Dar es Salaam, Shaaban Mkanza amefungua kesi ya madai ya Sh85 milioni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya Kampuni ya Usafirishaji mizigo ya DHL na Kampuni ya Bima ya Heritage kwa kushindwa kumlipa fidia baada ya kupata ajali akiwa kazini.
Kwa mujibu wa hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani hapo na wakili wa mdai, Semu Anney, mdaiwa wa kwanza anadaiwa Sh45 milioni wakati mdaiwa wa pili anadaiwa Sh40 milioni.
Wakili huyo alidai kuwa Mkanza alikuwa akifanya kazi ya kusafirisha vifurushi katika Kampuni ya DHL kwa kutumia pikipiki na kwamba alianza kazi hiyo Februari Mosi mwaka 2002 hadi Oktoba 2004.
Alidai kuwa mteja wake alipata ajali Julai 8 mwaka 2004 saa 5:45 asubuhi katika barabara ya Nelson Mandela na kuumia mguu.
Aliendelea kudai kuwa, baada ya kupata ajali hiyo alitibiwa kwa zaidi ya miezi mitatu hospitalini na baada ya hapo aliendelea na matibabu akiwa nyumbani takribani mwaka mmoja.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, mdaiwa wa pili ambaye ni Kampuni ya Bima ya Heritage, mdai anataka alipwe fidia ya Sh40 milioni baada ya kampuni hiyo kushindwa kumlipa fidia.
Alidai kuwa fedha hizo ni gharama ambazo zilitumiwa na familia yake kwa ajili ya kumpeleka hospitali kwa miezi minne, dawa na muuguzi wa kumhudumia nyumbani kwa muda wa miezi mitatu pamoja na gharama nyingine.
Katika kesi hiyo vielelezo mbalimbali vikiwamo ramani ya eneo la ajali, picha za mdai alipopata ajali pamoja na vyeti mbalimbali vya matibabu viliwasilishwa mahakamani hapo kama ushahidi.

Hakimu Mkazi Devotha Kisoka anayesikiliza kesi hiyo amepanga iendelee kusikilizwa Februari 20 mwaka huu ambapo Meneja wa Malalamiko kutoka Kampuni ya Bima ya Heritage Farh Dogo atatoa ushahidi.