Alitoa kauli hiyo alipokuwa akifunga Kikao cha sita cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) Chukwani mjini hapa mwishoni mwa wiki.
Alisema Zanzibar imekumbwa na migogoro ya ardhi hasa katika maeneo ya ufukwe wa bahari maeneo ambayo yamekuwa yakitumiwa na wawekezaji katika sekta ya utalii.
“Mheshimiwa Spika, hali hii ikiachiwa kuendelea tutaitumbukiza nchi yetu katika janga la uhasama miongoni mwa wananchi na hatimaye wananchi dhidi ya viongozi na serikali,” alisema.
Aliyataja maeneo yaliyokumbwa na mgogoro wa ardhi kuwa ni Pwani Mchangani, Kiwengwa, Nungwi na Mtende Kisiwani Unguja na Pemba.
Balozi Seif alisema sababu kubwa inayochochea migogoro hiyo ni kupanda kwa thamani ya ardhi hasa katika maeneo ya fukwe kutokana na kuimarika kwa sekta ya utalii.
Alisema wapo viongozi walafi wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya wananchi kupora ardhi za wakulima na wavuvi na kuuza kwa mamilioni ya fedha kwa wawekezaji wa kigeni na wazalendo.
“Kiongozi kazi yake kubwa ni kuonyesha njia ya matumaini kwa wananchi anaowaongoza, kiongozi anayeonyesha njia inayoelekeza kwenye uporaji wa ardhi hatufai,” alisema Balozi Seif.
Aliwataka Wajumbe wanaotoka katika maeneo yenye migogoro ya ardhi kuchukua hatua za kuwaelimisha Masheha na madiwani kuachana na vitendo vya utapeli vya kuuza ardhi kinyume cha sheria za nchi.
Balozi Seif alisema kwamba serikali haitovumilia Viongozi waliojingiza katika vitendo vya kupora ardhi wananchi na badala yake itahakikisha inawachukulia hatua kali za kisheria ili kuwa fundisho kwa viongozi wengine.
Tangu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Novemba, 2009, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar imepokea malalamiko 107 ya ardhi wakiwemo wakulima na wavuvi wanaolalamika kuporwa maeneo yao.
0 Comments