Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale.

Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, inatarajiwa kufumuliwa na kujengwa upya kwa kiwango bora cha lami ifikapo Mei, mwaka huu, baada ya ujenzi wake wa awali kubainika kuwa chini ya kiwango.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale, kutiliana saini mkataba na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaki Okada, kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kwa awamu ya pili.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo jana, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema kulingana na mkataba huo, mkandarasi kutoka Japana atakayejenga barabara hiyo atatumia gharama zake.
Waziri huyo alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo, ilitumia Sh. bilion 18.6, lakini serikali ilikataa kuipokea kutokana na kutojengwa katika kiwango kinachotakiwa na hivyo kusababisha kuharibika mapema.
Alisema ujenzi wa barabara hiyo katika awamu ya pili, utafanyika mwaka mmoja, utahusisha eneo la Bendera Tatu hadi Mbagala Rangi Tatu na baada ya kukamilika, mkandarasi atatakiwa kuiangalia kwa miaka miwili.

Dk. Magufuli alisema kutokea kwa tatizo hilo ni fundisho kwa wakandarasi wengine, ambao alitahadharisha kwa kuwataka wajiandae, hasa wale wanaofanya kazi bila kiwango.
Balozi Okada alisema matatizo yaliyojitokeza katika barabara hiyo ni ya kiufundi na kwamba wamekubaliana kuirekebisha.

Alisema mkandarasi huyo ataengeneza barabara hiyo kwa kiwango kinachotakiwa kutokana na makubaliano ambayo yaliyopo katika mkataba.

Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli aliwataka wakazi wa Mwenge na Morocco waliojenga nyumba katika hifadhi ya barabara kuondoka mara moja ili kupisha upanuzi wa barabara unaotarajia kuanza hivi karibuni.