YAPANDA KWA ASILIMIA 40.29, ONGEZEKO HALIWAHUSU WALALAHOI
Waandishi wetu
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imeidhinisha kupanda kwa bei ya umeme kwa asilimia 40.29 kuanzia kesho kutwa Januari 15 mwaka huu.Ongezeko hilo halitawahusu wateja wa hali ya chini, wanaotumia chini ya uniti 50 kwa mwezi pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), huku wafanyakazi wa shirika hilo wakitakiwa kulipa gharama za umeme kama watumiaji wengine.
Katika bei hizo, wateja wa hali ya chini wanaotumia chini ya uniti 50 kwa mwezi, bei itabaki kuwa Sh 60 kwa uniti wakati watumiaji wa majumbani wanaotumia zaidi ya uniti 50, bei hiyo itapanda kutoka Sh 195 hadi kufikia Sh 273 kwa uniti.
Watumiaji wa kawaida wakiwemo wenye biashara ndogondogo, bei imepanda kutoka Sh 157 hadi Sh 221 kwa uniti wakati watumiaji umeme mkubwa wa kati, bei imepanda kutoka Sh 94 hadi Sh 132 kwa uniti, wakati watumiaji umeme mkubwa hasa wenye viwanda na migodi, bei imepanda kutoka Sh 84 hadi Sh 118 kwa uniti na kwamba Zeco wamepandishiwa kwa asilimia 28.21 kutoka awali ambako, walikuwa wakilipa Sh 83 na sasa watalipa Sh 106 kwa uniti.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, alisema bei hizo hazihusishi kodi na kwamba Tanesco walitaka umeme upande kwa asilimia 155 lakini, baada ya mamlaka hiyo kuchambua maoni ya wadau, iliamua upande kwa asilimia 40.29 ili maisha yasizidi kuwa magumu.
Masebu alisema ongezeko hilo ambalo ni la dharura, litadumu kwa muda wa miezi sita na kwamba baada ya hapo, Ewura itafanya tathmini nyingine ya kujiridhisha juu ya huduma zinazotolewa na Tanesco na matokeo yake yanaweza kupandisha au kushusha gharama ya umeme.
Alifafanua kwamba kwa sasa kuna mtaalamu anayeangalia gharama halisi ya umeme kama ni halali ama la, ili kulinganisha na sababu za kupandisha gharama zilizotolewa na shirika hilo.
“Tumezingatia weledi wa hali ya juu, tumeona wanastahili japokuwa mambo mengine walisema ni dharura lakini baada ya kupitia, tumeona si dharura,”alifafanua Masebu.
Aliongeza, “Tumewapa uwezo Tanesco wazalishe umeme bila kuwa na mgawo na ikibidi, wakope ili waweze kuwa na mtaji mkubwa zaidi.”
Masharti
Alisema moja ya masharti waliyowapa Tanesco, ni pamoja na kuwataka kuanza kusambaza umeme unaozalishwa katika vyanzo rahisi kama maji na kwamba umeme huo ukipungua, ndipo waanze kutumia ule unaozalishwa kwa gesi, mafuta mepesi na mazito.
“Umeme unaozalishwa katika vyanzo vya maji una unafuu na tumewaeleza kwamba umeme huo ndio wanatakiwa kuanza kuutumia ila ukipungua ndio waanze kutumia unaozalishwa kwa gesi na mafuta,” alisema Masebu.
Akizungumzia upatikanaji wa vyanzo vingine vya umeme, alisema unatakiwa ufanyike kwa kutangaza zabuni ili wawekezaji waweze kupatikana kwa urahisi huku Ewura nao wakihusishwa katika uingiaji wa mikataba mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa Umeme katika mamlaka hiyo, Anastas Mbawala, alisema shirika hilo limetakiwa kutekeleza mambo mbalimbali ambayo yataboresha ufanisi ili wateja wapate huduma nzuri.
Kwa mujibu wa Mbawala, mambo hayo ni kuunganisha wateja wapya zaidi ya 100,000 kila mwaka, kuboresha mifumo ya usambazaji umeme ili kuondoa hali ya kukatikakatika mara kwa mara.
Alitaja mambo mengine kwamba ni kuhakikisha umeme unaopatikana usiwe hafifu, makusanyo yasipungue asilimia 96 kwa mwezi na mfanyakazi mmoja kuhudumia wastani wa wateja 172.
Alisema Tanesco pia wametakiwa kutoa ripoti kila mwezi na kwamba kutakuwa na mfumo wa elektroniki wa upashanaji habari ili kusiwe na matatizo ya kutofautiana kwa ripoti zitakazokuwa zinatolewa.
Mchango wa Serikali
Awali, Masebu alisema kutokana na Tanesco kutaka gharama hizo kupanda kwa kiwango cha asilimia 155, Serikali iliamua kuingilia kati suala hilo ikiwa ni pamoja na kutotoza kodi katika mafuta yanayotumika katika mitambo ya kuzalishia umeme.
“Serikali imefuta kodi ya mafuta kwenye mitambo ya IPTL sasa Serikali itakuwa inalipa Sh 18 bilioni na kusamehe deni la Sh 136 bilioni kwa Tanesco,”alisema.
Sababu za Tanesco
Masebu alisema sababu walizotoa Tanesco za kupandisha bei ya umeme ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mvua kunakosababisha upungufu mkubwa wa umeme na kuathiri hali ya kifedha ya shirika hilo na uchumi kwa ujumla, Ewura waliikataa.
Alisema hoja hiyo waliitupilia mbali, baada ya kuwasiliana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambayo iliwahakikishia kuwa hali ya mvua kwasasa ni nzuri.
Masebu alisema kutokana na uhaba wa mvua, Tanesco iliingia mkataba na kampuni ya IPTL kuzalisha megawati 100 kwa kutumia mafuta mazito, Symbion LLC kuzalisha megawati 112 kutumia gesi asilia na mafuta, pia ilisaini mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na Aggreko kuzalisha megawati 100 kutumia mafuta ya dizeli.
Alisema shirika hilo pia lilifafanua miradi yake ambayo itakamilika mwaka huu ambayo ni megawati 220 ambayo itatumia mafuta mazito (HFO) na gesi.
Alisema licha ya Tanesco kueleza kwamba mikataba hiyo imesaidia kupunguza mgawo wa umeme, pia ilieleza kuwa imeongeza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji wa Tanesco.
“Kutokana na hali hiyo, Tanesco iliwasilisha maombi ya dharura Ewura, ikiomba kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 155, ombi ambalo lilikubaliwa na Waziri mwenye dhamana ya umeme,”alisema.
Mkurugenzi huyo, alisema shirika hilo pia lilitaka madeni yake yaingizwe kwenye bei mpya ya umeme lakini Ewura ilikataa hoja hiyo.
Maoni ya Dk Slaa
Wakati Ewura ikibariki ongezeko hilo la bei ya umeme , Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa, amesema urasimu wa Serikali kutoruhusu watu na kampuni binafsi kuzalisha umeme, ndicho chanzo cha kuwepo bei kubwa za nishati hiyo nchini.
Dk Slaa aliyasema hayo juzi wakati akihutubia wananchi wa Jiji la Mbeya, katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nzovwe, ambako alisema tayari Bunge limeshapitisha sheria kuruhusu watu binafsi kuzalisha umeme lakini Serikali ndiyo haijaruhusu kutokana na urasimu wake.
Alisema hivi sasa Tanesco linafanya linavyotaka kwa kuwapandishia wananchi bei za umeme bila sababu za msingi kutokana na kukosa mpinzani katika biashara hiyo.
Dk Slaa alisema Serikali inatakiwa kuruhusu watu na kampuni binafsi kuzalisha nishati ya umeme, kama ilivyoruhusu kwa sekta zingine kumilikiwa na watu binafsi ili kuweza kuendelea kuzalisha umeme huo na kuchangia maendeleo mbalimbali ya kiuchumi nchini.
Alisema kwa kipindi kirefu, Tanesco inazalisha nishati hiyo lakini imekuwa ikifanya mambo inavyotaka bila kuangalia mustakabali wa watumiaji kwa kujipandishia bei za umeme itakavyo.
“Serikali inatakiwa kuondokana na ukiritimba huo na kutoa fursa kwa watu na kampuni binafsi kuzalisha nishati ya umeme kama inavyofanya kwa sekta zingine na sio kuendelea kuiangalia Tanesco pekee, kwa kuiachia kuzalisha umeme hali inayosabaisha utendaji mbovu katika sekta hiyo,” alisema Dk Slaa.
Alisema viongozi wa Serikali wanashidwa kubuni mbinu zitakazo wawezesha wananchi kuondokana na umasikini katika maisha yao, badala yake wanajali maslahi yao.
“Tatizo kubwa linaloisumbua Serikali yetu ni kwamba viongozi wanashindwa kuwa wabunifu wa kubuni na kubaini matatizo yanayowakabili wananchi wao, ndio maana miradi mbalimbali ya nchi imekufa wakati viongozi wapo, na hii ni sababu mojawapo inayosababisha kuwepo urasimu wa kutotoa fursa hiyo kwa watu na kampuni binafsi kuzalisha umeme,”alisema Katibu huyo wa Chadema.
Alisema wananchi wanaendelea kukubwa na adha kubwa ya kupandishiwa bei za umeme pasipo sababu za msingi, huku wengine wakiendelea kulala gizani kila mara kutokana na Serikali kushindwa kutoa uamuzi mgumu dhidi ya Tanesco na kushindwa kuruhusu watu binafsi kuzalisha umeme.
Habari hii imeandaliwa na Fidelis Butahe na Nora Damian, Dar, Godfrey Kahango,Mbeya.
0 Comments