Chama cha Wananchi (CUF) kimeandaa maadhimisho kukumbuka tukio la Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, la kuvunjwa mkono, wananchama wengine kadhaa wa chama hicho kujeruhiwa na kufunguliwa mashitaka ya uchochezi, mwaka 2001.
Tukio hilo lilitokea Januari 25, 2001 kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni (CUF), Frank Magoba, kwa lengo la kuhimiza maandamano ambayo yangefanyika Januari 27, mwaka huo.
Maandamano hayo yalikuwa na lengo la kudai mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tume huru ya uchaguzi na kutomtambua Amani Abeid Karume kama Rais wa Zanzibar.
Pia kushinikiza kurudiwa kwa uchaguzi Zanzibar na kupinga kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania enzi hizo, Benjamin Mkapa, ya kukataza maandamano na mikutano ya hadhara ya kisiasa.
Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na Siasa wa CUF, Shaweji Mketo, alisema jana kuwa maadhmishao hayo yatatanguliwa na maandamano ya amani.

Shaweji ambaye pia ni Katibu wa CUF Wilaya ya Temeke, alisema maandamano hayo yataanzia Mbangala Sababasaba Kwa Mpili na kuhitimishwa katika viwanja vya Zakhem, kuanzia saa 7 mchana.
Alisema maandamano hayo yatapokelewa na Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali.
Shaweji alisema viongozi mbalimbali wa kitaifa wa CUF watahutubia katika kilele cha maandamano hayo.
Alisema maadhimisho hayo yataenda sambamba na kumpongeza Profesa Lipumba kwa kuchaguliwa na Shirika la NED la nchini Marekani kuwa miongoni mwa wachumi wanaoshughulikia uchumi wa dunia.
Profesa Lipumba hivi sasa yuko nchini Marekani kwa miezi mitano.