Aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor(kushoto) alikuwa na uhusuiano rasmi na shirika la ujasusi la Marekani, CIA.
Mwandishi wa gazeti moja nchini marekani la Boston Globe, Bryan Bender, ameiambia BBC kwamba imemchukua miaka sita kupata jibu hilo kutoka kwa shirika hilo la CIA
Kulingana na mwandishi huyo, Bwana Taylor alipotoroka kutoka jela moja mjini Boston Marekani mwaka wa 1985, aliishi nchini Libya, ambapo aliweza kutafuta habari kuhusu marehemu Kanali Gadaffi na kuwasilisha maelezo yake kwa shirika la ujasusi la Marekani la CIA.

Bwana Bender amesema serikali ya Marekani ilithibitisha kuwa uhusuiano kati yake na Bwana Taylor ulianza miaka ya themanini.
Mwandishi huyo ameiambia BBC kwamba shirika la ujasusi la idara ya ulinzi limesema kuna stakabadhi nyingi za siri zinazothibitisha uhusiano kati yao na Bwana Taylor.
Lakini shirika hilo halikutoa maelezo zaidi kuhusu yaliyomo katika stakabadhi hizo.
Bwana Bender anasema aliwasilisha ombi kwa shirika la ujasusi la idara ya ulinzi na pia shirika la CIA miaka 6 iliyopita, akitaka kuelezwa ikiwa Bwana Taylor alikuwa na uhusiano wowote na mashirika hayo.