Rais Jakaya Kikwete akiweka udongo kwenye kaburi la aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema aliyezikwa katika makaburi ya Mkuya yaliyopo barabara ya Kivukoni kuelekea Ulanga, mjini Ifakara. (Picha na Ikulu).

MVUA KUBWA YAMSINDIKIZA HAYATI REGIA MTEMA

MVUA kubwa iliyoanza kunyesha mchana wakati ibada ya kumwombea marehemu Regia Mtema chini ya Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mahenge mkoani Morogoro Mhashamu Agapiti Ndorobo, ilivuruga kwa kiasi shughuli na utaratibu wa maziko yaliyofanyika mjini hapa jana.

Licha ya mvua hiyo kubwa kunyesha kuanzia saa nane mchana hadi saa 10 jioni mamia ya wananchi wa mjini Ifakara na wageni kutoka mikoa mbalimbali nchini wakiwamo wabunge wakiongozwa na Spika Anne Makinda, walishiriki kikamilifu ibada hiyo hadi mazikoni.

Rais Jakaya Kikwete alihudhuria maziko hayo ambayo yalifanyika kwenye makaburi ya
Mkuya katika barabara ya Kivukoni kuelekea Ulanga, na kabla ya shughuli hiyo, wananchi waliaga mwili wa marehemu kwenye uwanja wa Kiungani mjini Ifakara.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali kabla ya ibada hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, alisema Taifa limepoteza kiongozi shupavu
aliyekuwa akijenga hoja bungeni za kutetea wananchi bila kujali itikadi za vyama, dini au jinsia.
“Amefariki akiwa kiongozi kijana, msomi na nchi ilikuwa ikimhitaji kwa mchango wa mawazo yake na Serikali inatoa pole kwa wabunge, Spika na wananchi wa Kilombero na Morogoro pamoja na familia yake kwa kumpoteza kipenzi chao,” alisema Waziri Ghasia.



Spika Makinda alisema Regia alikuwa mtetezi mkubwa wa wafanyakazi wakiwamo wa kiwanda
cha Sukari cha Kilombero na kuwa kifo chake kimewashitua watu wengi na kukutanisha watu
wengi kutoka pande mbalimbali, wananchi na viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, wabunge wa vyama.

Alirudia kauli yake ya juzi Dar es Salaam, akisema Regia alionesha upendo na alikuwa nyota ya
upendo ya uwakilishi wa wananchi na ndiyo maana baada ya kifo chake amekutanisha watu
wengi kwa wakati mmoja Dar es Salaam na Ifakara.

Hivyo aliomba Watanzania, wamuenzi Regia kwa kufuata nyayo zake za upendo wa kila mtu
bila ubaguzi wa dini, jinsia au itikadi na wabunge walimpenda kutokana na ucheshi wake
ulioambatana na kutaniana kwa staha bila kujali rika la mtu.

Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, alimtaja Regia kuwa kiunganishi cha chama kwa vijana ndani na nje ya chama na alikuwa akitetea hoja alizokuwa akiziamini kuwa za kuleta maendeleo kwa Taifa, wananchi wake na chama chake, hivyo kimempoteza kiongozi muhimu na pengo lake halitazibika hata wakimpata mtu mwingine.

Hata hivyo, aliwahakikishia wananchi wa Kilombero, familia ya marehemu kuwa chama kitakuwa bega kwa bega katika masuala mbalimbali ya kijamii.
"Hatutaangusha wananchi wa Kilombero, wameonesha jinsi walivyokuwa karibu na Mbunge
wao, walivyokuwa wamempenda na hili limetudhihirisha kutokana na umati huu ... kutokana na upendo wake kwa kila mtu ... baada ya kifo chake, leo tumeona jinsi alivyotuunganisha, sisi kama chama, viongozi wa Serikali, wabunge na hili tutalizingatia katika kufanya uamuzi wetu
kwenye vikao," alisema Mbowe.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa Taifa pamoja na kuomboleza kifo cha Regia, alitumia fursa hiyo kuwaahidi wananchi wa Kilombero, kuwa chama kitaangalia jinsi ya kuwaondolea machungu ya kumpoteza kipenzi chao katika kumpata mwingine hata kama hataweza kufanana na marehemu kwa vitendo vyake.

Akitoa mahubiri wakati wa ibada ya misa ya kumwombea Regia, Askofu Ndorobo, alimtaja
kuwa mtu wa watu aliyeishi maisha ya kumcha Mungu na pia aliipenda nchi yake, ndiyo maana
alijitoa kutumikia wananchi wake na Taifa.

“Regia aliipenda nchi yake, aliipenda Kilombero na Watanzania wote, hivyo inatupasa tumwombee,” alisema Askofu huyo.

Hata hivyo, alisema pamoja na kuendelea kumhitaji, lakini mapenzi ya Mungu hayawezi
kupingwa na mtu yeyote hivyo ni wajibu wetu siku zote kuishi kwa kumcha Mungu.

Salaamu za Zitto
Akitoa salaamu za Chadema, Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto, alisema kuwa Regia nyota iliyozimika lakini kutokana na matendo yake, mwanga wake utaendelea kuangaza katika kuendeleza mapambano ya kuwakomboa Watanzania.

Akinukuu utenzi ulioandikwa mtandaoni na Mwanakijiji aliyesema kuwa alikuwa rafiki mkubwa
wa Regia na kusema kifo cha Regia ni pigo lililowaacha wote waliomfahamu, wakitetemeka,
kumlilia na machozi kuwadondoka.
“Lakini rafiki yako huyo kakuandikia shairi, uende ukisikiliza. Hapa tunalisoma kwa
kubadili sehemu fulani fulani, bila kubadili maudhui wala mtiririko wa mantiki, lakini swali letu kubwa ni je, unaweza kusikiliza?

“Basi sikiliza Regia, ukiweza tughani sote huu utenzi wa rafiki yako, usemao nyota imezimika,”
alisema Zitto.

Spika Anne Makinda alimsifia Regia kwa namna alivyoonesha uhodari katika shughuli zake kuwawakilisha wananchi, huku pia akiwa mcheshi kwa wabunge wenzake.