RAIS Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu na
kuhamisha Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kuanzia Alhamisi wiki hii.

Mabadiliko hayo yanamfanya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo, aliyekuwa amesimamishwa kupisha uchunguzi wa Kamati Maalumu ya Bunge, sasa kuondolewa kabisa katika nafasi hiyo.


Uteuzi huo ulitangazwa juzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, ikiwa ni siku moja kabla ya kuhitimisha mkataba wake wa utumishi wa umma uliomalizika jana na nafasi yake kuchukuliwa na Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.


Katika orodha ya walioteuliwa na kuhamishwa, Rais Kikwete amemteua Eliakim Maswi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini. Kabla alikuwa akiikaimu nafasi hiyo.


Jairo, tangu wakati wa Bunge la Bajeti katikati ya mwaka jana, alikuwa katika msukosuko akidaiwa `kuchangisha’ fedha za kulainisha bajeti ya wizara yake, jambo lililowakera wabunge.


Ili kupisha uchunguzi, Jairo alisimamishwa wadhifa wake na baadaye alirejeshwa, kitendo ambacho kilipingwa na hata Kamati iliyoundwa kuchunguza sakata hilo, nayo ilimkandamiza.Balozi Sefue alisema maendeleo ya nchi yanategemea utendaji mzuri katika sekta ya umma, hivyo ni lazima kila mfanyakazi awe mwadilifu na kutimiza majukumu yake ipasavyo.



“Mwekezaji au mfanyabiashara anategemea utendaji mzuri wa watumishi wa umma…utumishi wa umma ni tegemeo kwa kila kitu hivyo ni vyema kufanya kazi kwa kuangalia miaka 50 ijayo maana hata maendeleo ya leo yanatokana na kazi nzuri iliyofanywa miaka iliyopita,” alisema.

Naye Luhanjo alisema Balozi Sefue ni mtaalamu katika masuala ya utungaji sera, utumishi wa umma na demokrasia, hivyo anaweza kumudu vyema wadhifa huo mpya.

“Viatu vyangu si vikubwa sana kwake … nina uhakika atavimudu,” alisema Luhanjo na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha.

Hata hivyo, alisema Sefue anahitaji ushirikiano mkubwa kwa kuwa ameingia katika kipindi cha mchakato wa Katiba mpya, ambao unaambatana na changamoto nyingi katika uongozi.

Viongozi waliotoa maoni yao walisema Sefue ni mtu makini na anayejituma, hivyo wana imani kubwa kuwa atamudu changamoto za uongozi katika kipindi hiki cha uchumi unaotawaliwa na utandawazi na siasa ya demokrasia ya vyama vingi.

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema ingawa Sefue amefanya kazi serikalini kwa muda mrefu, si maarufu kwa kuwa amekuwa akifanya kazi kwa uadilifu mkubwa na si mtu wa kujikweza.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Utatibu), Stephen Wasira, alisema Sefue ni mchapa kazi hivyo watumishi wa umma wanapaswa kumpa ushirikiano wa kutosha kwa kufanyakazi kwa bidii na uadilifu.