Na Shakoor Jongo
Ndoa ya staa wa sanaa za maigizo Bongo, Nuru Nassor ‘Nora’ (pichani)inashikiliwa na nyuzi moja dhaifu kwa sababu yupo kwenye ‘gogoro’ zito na mume wake, Masoud Ali ‘Luqman’.
Habari kuwa Nora na Luqman hapatoshi, zimemiminwa kwenye gazeti hili na mnyetishaji wetu makini ambaye ameeleza kuwa chanzo ni kauli ya mrembo huyo aliyoitoa hivi karibuni.
Chanzo chetu kimeeleza kuwa kauli aliyoitoa Nora kuwa yupo tayari kuomba talaka endapo mume wake hatamruhusu kucheza filamu ndiyo iliyoibua ‘timbwili’ ndani ya familia hiyo yenye wanachama wawili.
“Mume wake aliposoma gazetini kauli ile, moja kwa moja alipitisha uamuzi wa kumuacha mkewe lakini ndugu wameingilia kati kunusuru ndoa hiyo,” alisema mtoa habari wetu na kuongeza:

“Hata hivyo, maelewano bado siyo mazuri. Wamesuluhishwa lakini mwanaume bado haelewi. Anasema Nora amemdhalilisha kupita kiasi na anaamaini hana mapenzi naye.”
Jitihada za paparazi wetu kumpata Luqman ziligonga ukuta lakini Nora alipovutiwa waya hewani, alikiri kuwepo kwa mtafaruku mzito na mume wake.
“Naumia sana, sikutegemea kama yale maneno yangemuudhi mume wangu na watu wengine, kwa sasa nipo katika hali ngumu ya kuweka mambo sawa ili nieleweke kwamba sikuwa na nia mbaya.
“Watu wananiona kituko, familia yangu hainielewi, najuta kwa nini nilitoa kauli ile, naomba nichukue nafasi hii kuomba radhi kwa kila mtu aliyekwazika na kauli niliyoitoa,” alisema Nora.