Mtu mmoja amekufa na wengine 15 wamelazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Iringa Vijijini ya Ipamba baada ya kula nyama ya ng’ombe inayodhaniwa kuwa na sumu.
Tukio hilo lilitokea Januari 25, mwaka huu katika Kijiji cha Kibebe, Kata ya Ulanda, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini.
Imeelezwa kwamba wananchi hao walinunua nyama ya ng’ombe aliyekufa na kuitumia kama kitoweo.
Habari zilizopatikana jana kijijini humo na kuthibitishwa na Afisa Mtendaji wa Kata hiyo (WEO), Humphrey Kisika, zilieleza kuwa aliyefariki dunia kwa kula nyama hiyo yenye sumu ni Titus Mwilapa (70).
Inadaiwa kuwa mkazi wa kijiji hicho, Juliana Lweve (75), alikata kata na kuuza mzoga wa ng'ombe mdogo (ndama) na kuwauzia wananchi wenzake.
Aidha, Mtendaji huyo aliwataja walionusurika kufa na kukimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya Ipamba kuwa ni Machelina Kihaga, Anna Sekilongumtwa, Baraka Mgongolwa na ndugu wawili wa familia moja, Bartholomew Chatila na Oswald Chatila.
Wengine ni Chelimo Msofu, Kisongo Kigeleso, Margareth Nyakunga, Beatrice Sambala, Margareth Pancras na wengine waliotambuliwa kwa jina moja moja la Gift, Mpesa, Wugi, Mgongolwa na Yusuph.
Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Evarist Mangalla, alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, alisema kuwa Mwilapa (marehemu), alifariki dunia juzi saa 8:30 mchana wakati akipelekwa kupata matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Ipamba.
“Huyu marehemu yeye alifariki dunia akiwa katika kitongoji cha Ikolima na inasadikiwa alikula nyama ya ng’ombe mwenye sumu ambaye alikuwa amekufa, wananchi wengine 15 walikwenda kupata matibabu lakini baadhi yao wameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya hali zao kuwa nzuri,” alisema Kamanda Mangalla.
Kufuatia hali hiyo, Kamanda Mangalla alisema kuwa Polisi mkoani hapa inamshikilia mwanamke Lweve (75), anayedaiwa kuuza mzoga huo.picha haihusiani na maelezo.