Rais wa MAT, Dk. Namala Mkopi, akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.Kulia ni Dr. Rodrick Kabangila.

 Ni baada ya wenzao 229 kutimuliwa
Wasema wagonjwa wengi wanakufa
Ni kwa kukosa huduma za matibabu

Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimechachamaa na kusema kitendo cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwaondoa madaktari 229 katika wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kimeathiri upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa na kusababisha kutokea vifo vingi kwa kukosa matibabu.
Kadhalika, MAT kimesema huduma katika hospitali hiyo kubwa nchini zimezoroka kwa kiwango kikubwa kutokana na madaktari wachache waliopo kushindwa kukidhi kutoa huduma ya matibabu hata nusu kwa kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo.
Hayo yalisemwa jana na Rais wa MAT, Dk. Namala Mkopi, wakati wa mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Dk. Mkopi alisema kuwa kitendo cha madaktari hao kupewa barua ya kurejeshwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii huku maelfu ya Watanzania wakihitaji huduma yao ni cha hatari kwa kuwa kimeathiri utendaji na upatikanaji wa huduma za afya hospitalini hapo.

" Hatua ya Mkurugenzi kuwaandikia barua ya kuwataka wakaripoti wizarani wakati maelfu ya Watanzania wanahitaji huduma yao huku wengine wakipoteza maisha kwa kukosa matibabu kwa wakati kutokana na upungufu wa madaktari ni unyama wa hali ya juu kwa walalahoi,” alisema na kuongeza kuwa:
“Chama kimeguswa na kusikitishwa na hatua iliyochukuliwa ya kuwafukuza kazi madaktari hao, hakuna sababu ya kukomoana wala kutishiana wakati mtu anapodai haki yake ya msingi basi cha muhimu ni kushirikiana ili Watanzania wote wapate haki yao ya msingi. Kuingiza siasa na kuchanganya na taaluma ya afya haifai.”

Alisema watu wachache walioko wizarani wanafanya maamuzi kwa lengo la kuwakomoa madaktari hao kwa sababu ya kudai haki ya msingi.
“Inasikitisha kiongozi anasema eti sio madaktari ni wanafunzi, ni dharau kubwa hawa ni madaktari ambao wamehitimu na kula kiapo cha utii, itakuwaje mtu anasema hawana sifa wakati wanatoa huduma zote zinazostahili na ndiyo sababu Serikali imewapangia kufanya kazi katika hospitali hii?” alihoji.
“Isitoshe, wanaipenda kazi yao, walipoingiziwa fedha kwenye akaunti walipata nauli za kwenda kazini mara moja kuwatumikia Watanzania, ” alisema.
Alisisitiza kuwa wakati mwingine Rais Jakaya Kikwete, amekuwa akilaumiwa matukio yanapotokea na kusisitiza kuwa kwa upande wa suala la madaktari, serikali haihusiki bali ni Katibu Mkuu na Mganga Mkuu wa Wizaya hiyo wanaoharibu taaluma ya afya.
Dk. Mkopi alisema mapema wiki iliyopita, uongozi wa chama hicho ulikutana na wa wizara hiyo kuzungumzia suala la kuwalipa madaktari hao madai yao ili waendelee na kazi, lakini cha kushangaza wamewafukuza kazi wakati wakiwa wamerejea kazini baada ya kulipwa haki zao.
Katibu wa MAT, Dk. Rodrick Kabangila kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza, alisema siasa imeingia katika taaluma ya afya na kwamba madaktari hao hawakugoma bali walikosa nauli na fedha ya chakula.
WAENDA KWA PINDA
Alisema chama hicho kimepeleka malalamiko kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na kwamba Jumamosi ijayo kutakuwa na mkutano wa dharura wa madaktari wote nchini ambao watautumia kutoa tamko lao rasmi kuhusu tukio hilo.
Alhamisi iliyopita, serikali ililipa fedha za madaktari 229, lakini Ijumaa waliamriwa kuondoka Muhimbili na kutakiwa kuripoti wizarani ili wapangiwe vituo vingine kwa madai kuwa wamekiuka mkataba wao wa kazi.
Uongozi huo uliwataka madaktari hao kuhakikisha wanarudhisha vifaa ambavyo wamepatiwa na hospitali hiyo ikiwemo funguo za vyba na vtambulisho kisha kuripoti wizarani hapo mara moja.
Madaktari hao walikuwa wanaidai serikali Sh. milioni 176 za posho zao za kujikimu ambazo zilicheleweshwa na kusababisha madaktari hao kuishi katika mazingira magumu.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kulipwa fedha zao na kurejea kutoa huduma wodini, waliamriwa kuripoti katika ofisi za utawala za hospitali hiyo ambako walipatiwa barua za kurejeshwa wizarani.
NIPASHE ilifanikiwa kuipata barua hiyo ambayo ilisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk. Marina Njelekela ikieleza kuwa uamuzi huo umefanywa na makubaliano ya uongozi wa hospitali hiyo.
Moja ya kipengelea cha barua hiyo ilisomeka kuwa: “Uamuzi huu umechukuliwa baada ya wewe kukiuka makubaliano ya mafunzo kwa vitendo baina yako na hospitali ya Taifa Muhimbili, kifungu namba 1 (b), (d), (f) na (g) kama ilivyoelekezwa na Katibu Mkuu katika barua yake ya kukupangia mafunzo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.”
“Sisi hatujafanya mgomo kama inavyodaiwa ila tunachokijua ni kwamba hatujaingia kazini kutokana na kwamba hali zetu sio nzuri katika masuala ya kifedha na ndio maana wengine iliwawia vigumu kuendelea na kazi mpaka hapo watakapopatiwa posho zao na tulivyopatiwa fedha zetu juzi jioni tulianza kazi tunashangaa kupatiwa barua ya kufukuzwa,” alisema Dk Deogratus Mally ambaye ni kiongozi wa madaktari hao waliofukuzwa.
Dk. Mally alisema kuhusiana na jambo hilo la kudaiwa wamevunja mkataba, watatafuta mwanasheria ili kulijadili na kusisitiza kuwa hawapo tayari kwenda kuripoti wizarani.
Alisemakwa sasa wanajiandaa kumuandikia barua Mkurugenzi wa MHN kumjulisha kuwa hawajavunja mkataba kama alivyodai.
“Wao wametuvunjia mkataba wetu kwa kutucheleweshea fedha kwani makubaliano ni kwamba kila mwisho wa mwezi tunapatiwa posho zetu na hawakutujulisha kama fedha zetu zitachelewa halafu wanatubadilishia kibao kuwa sisi tumevunja mkataba hivyo basi hatupo tayari kuripoti wizarani,” alilalamika.
Aisema hawakugoma mgomo, isipokuwa wanachojua ni walimuandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, kumjulisha kuwa walishindwa kwenda kazini kwa kukosa fedha za usafiri na mambo mengine.