JUMUIYA ya Khoja Shia Ithnasheri Jamaat, inajipanga kuchangia damu mara mbili kwa mwaka ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayepoteza maisha kwa kukosa damu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa mpango wa kujitolea damu kutoka jumuiya hiyo, Fazleabbas Dhirani, alisema kuwa wamekuwa na utaratibu wa kuchangia damu kila mwaka ili kupunguza tatizo la upungufu wa damu nchini.
Alisema kuwa Tanzania ina uhitaji wa damu na ingawa kuna watu wengi wanao uwezo wa kuchangia, hawafanyi hivyo kutokana na mipangilio na utamaduni uliojengeka katika wanajamii.
“Jamii inashindwa kujitolea damu kwa kuogopa kutambua afya zao bila kujua kwamba kujitambua afya ni jambo jema, sasa sisi jumuiya yetu tuna wanachama ambao kila mwaka tunachangia damu,” alisema.
Alisema damu hiyo husambazwa kwenye hospitali mbalimbali nchini kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wenye uhitaji wa damu bila malipo.
Kwa mujibu wa Dhirani, wakati wa kuchangia damu hushirikiana na wataalamu mbalimbali kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na ofisi ya Mpango wa Damu Salama.
Dhirani alisema kuwa Watanzania wengi hufikiri kwamba suala la kuchangia damu ni mpaka apate mgonjwa na kuwataka kuachana na mawazo hayo na badala yake wajenge utamaduni wa kujitolea damu mara kwa mara ili kuhakikisha hospitali zote nchini zinakuwa na damu za kutosha.
Pia alizitaka taasisi na jumuiya mbalimbali nazo kujitolea damu ili kuwasaidia watu wenye uhitaji na kufikia lengo.
0 Comments