Wananchi na viongozi mkoani Kigoma wametahadharishwa kuwa macho na wahamiaji haramu na wageni toka nje ya nchi wakati wa kutoa maoni ya katiba mpya. Tahadhari hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Danh Makanga katika mkutano wa hadhara wa uhamasishaji wananchi kujitokeza kwa wingi wakati ukifika kutoa maoni .
Amesema kufuatia kuwepo kwa maelfu ya wahamiaji haramu katika mkoa wa Kigoma na mwingiliano mkubwa wa wananchi toka Burundi na Kongo DRC, wananchi wanatakiwa kuhakikisha raia hao wa nchi jirani hawapati nafasi ya kuchangia kwa kuwa ni kinyume cha sheria.
“Nawaomba sana, kama mnavyojua tunajua Warundi wengi na Wakongo hapa kwetu, wamo vijijini mwetu na mijini, sasa wakati ukifika tuwe makini wasipate nafasi kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumenusuru kupata maoni ya nchi zao kwenye katika yetu,” alisema.
Alisema mwingiliano mkubwa wa raia toka nchi jirani kuna uwezekano mkubwa kwa wageni kujipenyeza na kutoa maoni katika tume, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha kuwa wageni hawapati fursa hiyo kwani wanaweza kupendekeza vitu ambavyo si mahitaji ya Watanzania.
Mkoa wa Kigoma una zaidi ya wahamiaji haramu 1000 toka Burundi na Kongo (DRC) wanaoishi kinyume cha sheria katika maeneo mbalimbali mkoani hapa .
Naye Mbunge wa viti maalum CCM kupitia mkoa wa Tabora, Munde Tambwe, amesema fursa ya wananchi kutoa maoni ikitumiwa vizuri itawezesha masuala mbalimbali yanayolalamikiwa kupatiwa ufumbuzi.
“Wananchi wenzangu tusiwe watu wa kulalamika tu , fursa inakuja tuotumie vizuri kuhakikisha tunayoyataka yanakuwemo na hakuna namna ya kuhakikisha tunayoyataka yanakuwemo kama kushiriki kutoa maoni tume itakapopita,’’ alisema.