Na Imelda Mtema
CHIPUKIZI anayeonesha nia ya kuwaangusha wakongwe katika Tasnia ya Filamu Bongo, Kajala Masanja, yupo hoi taabani hospitalini, Risasi Mchanganyiko linakuhabarisha kwa majonzi.
Awali, habari zilitua mezani mwa gazeti hili kutoka kwa chanzo chetu makini, ambacho siku zote hutonya ‘nyuzi’ zisizo na shaka, kwamba mlimbwende huyo ni mgonjwa.
“Kajala anaumwa, amelazwa. Yupo kwa Kairuki (Dk. Kairuki). Hali yake, mh! Anahitaji kuombewa,” kilieleza chanzo hicho.
KAZI IKAANZA
Dawati la Risasi Mchanganyiko lilimteua mwandishi wa habari hizi, kufuatilia kwa makini suala la afya ya Kajala ambapo haraka alianza kuwasiliana na baadhi ya wasanii ambao wapo karibu na msanii huyo.
“Ni kweli Kajala anaumwa, anasumbuliwa na tumbo. Kwa kweli ameanza mwaka vibaya sana,” alisema mmoja wa watu wa karibu naye kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini.
RISASI MZIGONI
Baada ya kujiridhisha na maelezo ya wasanii kadhaa, Polisi wa Risasi Mchanganyiko, alifunga safari hadi katika Hospitali ya Kairuki, Victoria jijini Dar es Salaam kumtembelea msanii huyo.
Kweli, gazeti hili lilimkuta Kajala akiwa amelazwa katika hospitali hiyo.
ANASUMBULIWA NA NINI?
Akiongea kwa taabu hospitalini hapo, Kajala alisema anasumbuliwa na tumbo kwa muda mrefu sasa na limekuwa na kawaida ya kupona na kuanza tena kuuma kwa mpishano wa vipindi vifupi.
“Hili tumbo linaninyima raha sana...(anataja jina la mwandishi). Yaani likinishika huwa napata maumivu makali mno. Hata hivyo, namshukuru sana Mungu, sasa hivi naendelea vizuri,” alisema Kajala na kuongeza:
“Madaktari wameshauri nifanyiwe vipimo vya Ultrasound na X-Ray ili kujua nina tatizo gani tumboni. Wameniambia baada ya majibu ya vipimo hivyo, watajua pa kuanzia.”