Musa Mateja na Richard Bukos SIRI ya mwanaume Mzungu (jina halikupatikana mara moja) aliyefariki dunia Januari 21, mwaka huu akiwa ndani ya chumba alichopanga kwenye hoteli moja iliyopo Sinza, jijini Dar es Salaam imefichuka, Ijumaa Wikienda limeinyaka.
Kwa mujibu wa chanzo chetu ambacho kinafanya kazi kwenye hoteli hiyo, usiku wa kifo chake, mwanaume huyo alitoka kwenda matembezini, aliporudi alikuwa ameongozana na msichana wa Kitanzania aliyekuwa akizungumza Kiingereza vizuri.
“Usiku yeye alitoka, sijui alikwenda wapi? Aliporudi alikuwa na msichana mzuri tu, naamini ni Mtanzania maana alisalimia Kiswahili, lakini pia alikuwa akiongea Kiingereza vizuri na marehemu,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa wawili hao walionekana kuwa na amani muda wote wa mazungumzo yao lakini cha kushangaza, asubuhi mwanaume huyo alikutwa amefariki dunia chumbani akiwa peke yake.
Aidha, nje ya hoteli hiyo, baadhi ya watu waliokuwa wakishuhudia mwili wa marehemu ukiingizwa ndani ya gari la polisi, Land Rover lenye namba za usajili T 760 ADY walisikika wakisema huenda mrembo aliyekuwa na mtasha huyo alimwekea madawa ya kulevya kwenye kinywaji ili amwibie fedha.
“Kama alikuwa na hawa mademu wetu wa Kibongo, usikute alimwekea madawa ya kulevya ili amwibie hela zake, sasa kila mtu na afya yake, mwingine analewa tu, mwingine anakufa kabisa,” alisema shuhuda mmoja baada ya kusikia minong’ono ya kuwepo kwa mwanamke usiku wa tukio.


Kwenye tukio kama hilo hapakauki maneno, shuhuda mwingine alidai kuwa yeye alilala kwenye chumba kimoja hotelini hapo na anaamini marehemu alipewa mambo makubwa na mrembo huyo hadi kufikia hatua ya kupoteza fahamu hatimaye kifo.
“Kama kweli alikuwa na demu Mbongo basi alipewa mambo mazito ya Kiafrika, kama afya ya Mzungu ilikuwa inazingua matokeo yake ndiyo haya. Mbona wanaume wengi tu wanakufa wakifanya tendo la ndoa,” alisema shuhuda huyo.
Ijumaa Wikienda liliwauliza askari waliofika kuuchukua mwili huo nini kilimuua marehemu, lakini waligoma wakidai wao si wasemaji wa jeshi la polisi na mwenye dhamana ya kutoa maneno kwa waandishi ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Afande Suleiman Kova.
Aidha, askari hao waliondoka na rafiki wa kiume wa marehemu ambaye naye ni Mzungu kwa madai ya kuisaidia polisi katika upelelezi wao.
Hata hivyo, habari zinasema kwamba wawili hao walifika pamoja kwenye hoteli hiyo, lakini kila mmoja alipanga chumba chake.
Kamanda Kova hakupatikana Jumamosi kuzungumzia sababu ya kifo hicho baada ya simu yake ya mkononi kuita muda mrefu bila kupokelewa.