Na Gladness Mallya
 KWA mara ya kwanza tangu gogoro la kindoa lililopoibuka kati ya mwanaye, Irene Uwoya na mwanasoka wa Rwanda, Hamad Ndikumana ‘Kataut’, mama mzazi wa staa huyo, Naima Uwoya, amenena mazito juu ya ishu hiyo, ni Ijumaa Wikienda pekee lenye mkanda kamili wa alichokisema.
MASIKITIKO
Akizungumza ‘eksiklusivu’ na gazeti hili nyumbani kwake Mbezi Jogoo, Dar es Salaam, hivi karibuni, mzazi huyo alionesha kusikitishwa na mgogoro huo kwa maelezo kuwa uliitia aibu familia ya Uwoya.
Mama wa Uwoya aliweka wazi kuwa hana taarifa rasmi za kuvunjika kwa ndoa hiyo kwa sababu jambo kama hilo lina taratibu zake hasa katika dini ya Kikristo, hivyo Irene au Ndikumana, hakuna mwenye uwezo wa kutangaza kuvunja ndoa hiyo.
HAJAONA TALAKA
“Ndoa gani imevunjika? Mbona sijaona talaka? Ninachojua si Irene wala Hamad (Ndikumana) mwenye uwezo wa kusema ndoa imevunjika bila kufuata taratibu zilizowekwa,” alisema mama Uwoya.
Mzazi huyo aliendelea kudadavua kuwa katika ndoa yoyote ile lazima hali ya kutofautiana itokee kutokana na mitazamo wa wahusika katika jambo fulani.
“Hata kwa Irene na Hamad, ndicho kilichotokea, lakini sina habari ya kuvunjika kwa ndoa yao.

IRENE ANAPONZWA NA MARAFIKI
Kwa mujibu wa mama Uwoya, matatizo ya kindoa yaliyompata Irene yalitokana na kuponzwa na rafiki zake kwa sababu baadhi yao siyo wazuri, wana tabia ya kuzungukana.
IRENE SIKIO LA KUFA?
Mzazi huyo alisema amekuwa akimsihi Irene mara kwa mara awe makini na mtu anayejenga naye urafiki kwani rafiki asiyemtegemea ndiye atakayemgeuka baadaye.
Alisema ameshamkanya aangalie upya mwenendo wake kwa sababu mume siyo mtu wa kuchezeachezea na hakuna aliyemlazimisha kuolewa, alikubali mwenyewe kwani ndiye aliyempeleka na kuwatambulisha wao kama wazazi, wakawauliza maswali, waliporidhia ndipo ndoa ikafungwa.
Alitoa dukuduku la moyoni kwa kusema kuwa ameshamshauri hata juu ya filamu anazocheza aepuke kujiachia sana kama ilivyokuwa zamani kwani kwa sasa ni mke wa mtu na ana mtoto hivyo anatakiwa kujiheshimu.
Mama Uwoya alimalizia kuwa mambo hayo yote hayaleti picha nzuri na Irene siyo mtoto mdogo hivyo amuondolee aibu anayokumbana nayo mitaani na simu anazopigiwa juu yake.