Mkuu wa wilaya ya Bahi Betty Mkwasa akiwa na wanafunzi waliopata ufadhili wa masomo Teddy Mhala (kushoto), Joyce Nonyo na Julliet Chahoza.

TATIZO la mimba shuleni ambalo limekuwa likisababisha wasichana wengi kuacha shule na hivyo kuzima ndoto za mafanikio yao, linaelekea kutoweka Wilaya ya Bahi Mkoa wa Dodoma kutokana na juhudi mbalimbali zikiwemo zile zilizofanywa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Betty Mkwasa.

Mkuu huyu wa Wilaya alipoingia katika wilaya hii na kukuta tatizo hili akitambua kwamba kumwelimisha mwanamke ni kuelimisha jamii alimua kuwavaa wazazi na walezi ili kuondoa tatizo hilo ambalo lilishajenga utamaduni na kuonekana la kawaida na si kitu cha kuuliza.

Tatizo la wanafunzi wa kike kukatisha masomo huku wahusika wa mimba hizo wakiwa hawajulikani kutokana na wasichana kutowataja wahusika, lilifanya mazingira ya kumkomboa mtoto wa kike kuwa magumu zaidi.

Falsafa ya wakazi wa Bahi ililenga kuwaokoa wanaume hao kwa hofu kwamba watakamatwa
na kufungwa na kugombanisha koo. Hali hiyo ikaongeza ukubwa wa tatizo kutokana na wasichana wengi kupoteza mwelekeo baada ya kukatisha masomo.

Pia wilaya hiyo ilikuwa na tatizo kubwa la watoto kutozingatia masomo lakini hali hiyo kwa sasa inaonekana imekwisha. Kulingana na Mkuu wa Wilaya hiyo, alipofika Wilaya ya Bahi miaka mitatu iliyopita kulikuwa na idadi kubwa ya watoto waliokuwa wakiacha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro na tatizo la mimba.

Utoro ulikuwa ukisababishwa na tabia ya kuhamahama kwa wafugaji kutafuta malisho ambapo
wakati mwingi walikuwa wakihama na familia zao. “Kwa wafugaji wengi suala la elimu halipewi kipaumbele, nilianza na mkakati wa kuhakikisha utoro unapungua, niliunda vikundi vya msukumo kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Tarafa na hata Wilaya “ anasema.



Katika zoezi hilo kulikuwa na kufuatilia pamoja na kukamata wazazi ambao watoto wao walikuwa hawafiki shuleni. “Kilichofanyika ni kumkamata mke au mume, na aliyekamatwa
kati yao hawezi kuachiwa mpaka aseme mtoto wake yuko wapi na anakwenda kumleta.

Hilo kwa kiasi kikubwa ilisaidia kwani wazazi walienda kuwaibua watoto walipo.” Alisema Betty. Mkuu huyo wa Wilaya anabainisha kuwa, katika kipindi cha mwaka 2011, jumla ya wanafunzi 460 walifanikiwa kurudishwa tena shuleni.

Wazazi na walezi wakaogopa na kuanza kufuatilia maendeleo ya watoto wao baada ya kuona
mkono wa sheria ukiwaelemea. Na kurejea kwa watoto hao shuleni kumefanya pia kubadilishwa kwa msimamo wa kifalsafa ili taratibu falsafa ya kuogopa mkono wa dola
kubadilika na umuhimu wa elimu kuonekana.

“Kiukweli juhudi hizi zimefanya tuwe wa pili kimkoa, “ alisema Betty ambaye katika mahojiano
alionesha kuridhishwa na hatua waliyofikia wilaya na wakazi wake katika masuala ya kuthamini
elimu kwa watoto hasa mtoto wa kike.

Licha ya juhudi hizo aliona ipo haja ya kuwapa mikakati ya kujihami watoto wa kike ili wasidanganyike na maisha na hivyo kuharibikiwa kwa kupata mimba au kutoroka shule kwenda kutafuta fedha.

Miongoni mwa mbinu iliyotumika kubakiza wanafunzi kwenye msimamo ni kuanzisha klabu za
wanafunzi mashuleni. Anasema Mpango wa kuanzisha klabu za wanafunzi wasichana katika shule za msingi na sekondari wilayani Bahi umekuwa na mafanikio makubwa.

Klabu hizo zilianzishwa katika shule 21 za msingi na sekondari na uzinduzi wake ulifanywa na
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Ummy Mwalim. “Tulipita shule zote na nilishirikiana na maofisa Elimu, na madiwani viti maalumu wanane , nilitaka kwenye ngazi za Kata wawe walezi tuliwafundisha jinsi ya kuwa wajasiri” anasema.

Ukweli ni kuwa mtu akiwa jasiri na kujiwekea malengo hakuna wa kumdanganya, katika ziara
hiyo tulipata wanafunzi waliokiri kuwa elimu hiyo wangekuwa wakiipata tangu wakiingia shuleni wangekuwa na ujasiri na wasingekuwa watu wa kuyumbishwa.

Lakini kabla ya uzinduzi huo tayari shule mbili za Chibelela na Chipopelo zilikuwa tayari
zimezindua klabu zake. Pia kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wanafunzi kuwa baadhi ya walimu walikuwa wakiwataka kimapenzi jambo ambalo lilileta usumbufu kwao.

Tuliwafundisha wasichana namna ya kuepuka vishawishi na hivyo kupunguza tatizo lililokuwepo la kutakwa kimapenzi na watu mbalimbali wakiwemo walimu ambao walikuwa wakiwafundisha.

Tuliwafundisha namna ya kujitambua na madhara yatakayopatikana na kufanya ngono wakiwa na umri mdogo, elimu hiyo ilisaidia kwani wengi wakafunguka masikio na hata wale waliokuwa hawafahamu madhara wakajifunza namna ya kujitunza ili kuepukana na ngono zisizo salama ambazo pia husababisha maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Tulimuomba Naibu Waziri atusaidie kupata vipeperushi juu ya maisha ya ujana na malezi kwa
ujumla na hata vile vinavyozungumzia maradhi ya ngono. Katika klabu hizo kuna kwaya,
ngoma za asili, kuna michezo mbalimbali kuna wakati tunagawa mipira lakini ninahangaika
kutafuta wafadhili.

Pia tulitengeneza katiba mwanachama yoyote anapoingia kidato cha kwanza ahakikishe anafika kidato cha nne, pia awe na nidhamu, avae nguo za heshima, mwenye uwezo wa kujieleza, mjasiri pia asiwe mtoro.

Juhudi hizo zikasaidia kupungua kwa tatizo la wanafunzi kupata mimba katika Wilaya ya Bahi.
Sababu nyingine waliyogundua ni kuwa, wazazi wengi walikuwa wakiambia watoto wao wasifanye vizuri shuleni ili wafeli na hapo mtoto atumike kama kitegauchumi cha kuingizia kipato familia.

Kaya nyingi zilionekana zilikuwa zikiwaoza watoto wakiwa na umri mdogo na wengine kwenda kufanya kazi za ndani nje ya Wilaya ya Bahi. Tatizo hili lilimalizika baada ya wazazi kuelimishwa umuhimu wa elimu kwa watoto wao jambo lililosaidia hata kuongeza kiwango cha ufaulu katika Wilaya.

“Wazazi wengine walikuwa wakitishia kuwapiga watoto wao au kuwafukuza nyumbani iwapo watafanya izuri shuleni jambo ambalo lilifanya watoto wengi wasizingatie masomo kutokana na vitisho kutoka kwa wazazi wao” anasema.

Anazitaja juhudi nyingine ni kuhakikisha kuwa,anatafuta udhamini kwa wanafunzi ambao wanafaulu vizuri ili kuwawezesha kuwa mabalozi wazuri kutoka katika Wilaya ya Bahi. Juhudi hizo zinaonekana kuzaa matunda baada ya wanafunzi watatu wa kike waliofaulu vizuri katika masomo na kupata udhamini.

Anasema kuwa, anapenda kuona wasichana zaidi kutoka Wilaya ya Bahi wanasoma masomo ya sayansi na hili litamtia moyo kwa kushawishi wafadhili wengine. Udhamini huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya kutengeneza mvinyo ya Cetawico, Fiorenzo Chesini na utagharimu Sh milioni 24.

Wasichana waliopata udhamini huo ni wale waliomaliza darasa la saba mwaka jana na kufaulu vizuri katika masomo ya Hisabati na Kiingereza ambapo wanafunzi hao watalipiwa ada kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne katika Shule ya Kimataifa ya Kilimanjaro Academy.

Wanafunzi hao ni Teddy Mahala (14), Joyce Nonyo (13) na Julieth Chahonza (13) ambao
walikuwa wakisoma shule za Zanka na Chibelela katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Kati ya wanafunzi hao, Teddy ni yatima ambaye hana baba wala mama.

Kulingana na mlezi wa Teddy ambaye ni mwalimu katika Shule ya Msingi ya Zanka, Egla Mgubesi, ni kuwa, Teddy amekuwa akishika namba moja darasani kuanzia darasa la kwanza mpaka alipomaliza darasa la saba.

Mwalimu Mgubesi anasema kuwa, amefarijika kwa udhamini uliotolewa kwa mtoto huyo yatima ambaye anapenda kusoma na sasa atatimiza ndoto zake. “Nashukuru kwa ajili ya ufadhili huo, pia natoa shukrani zangu kwa Mkuu wa Wilaya kutokana na juhudi alizofanya, Mungu awajalie wote waliohusika,” anasema mwalimu huyo.

Akielezea alivyopata ufadhili kwa wanafunzi hao Mkuu wa Wilaya Betty alisema kuwa, aliandika barua kuomba ufadhili kwa ajili ya wanafunzi wawili lakini jambo la kushangaza Cetawico ilitoa udhamini kwa ajili ya wanafunzi watatu na pia wameahidi kutoa ufadhili kwa mwanafunzi mwingine mmoja ambaye ni mvulana.

Anasema kuwa, hilo likamtia moyo kwani lengo lake la kuhakikisha watoto wa kike wanapata kipaumbele katika suala la elimu likatimia lakini atafurahi zaidi kama wadhamini wengine watatokea ili kuweza kusaidia suala zima la elimu katika Wilaya ya Bahi.

Paula Nkane ni Ofisa elimu Sekondari katika Wilaya ya Bahi, anasema kuwa kwa sasa kuna mwamko mkubwa wa elimu katika Wilaya ya Bahi kutokana na juhudi za viongozi wa Wilaya.
Anabainisha kuwa, katika Wilaya ya Bahi mwaka jana wanafunzi 120 walichaguliwa kujiunga na shule za sekondari za bweni kati yao wasichana ni 36.

Ni wazi kuwa juhudi hizo zikiendelea na hata kuibuliwa kwa mbinu mpya kwa kiasi kikubwa itasaidia kuongeza idadi ya ufaulu katika shule za msingi na sekondari na hata kuinua hali ya elimu kwa ujumla katika Wilaya ya Bahi.
                                      chanzo cha habari.