Na Brighton Masalu
KILIO, maumivu, usaliti na ulaghai vinazidi kuvuma kwa kasi ya pepo za kusi katika mapenzi ya mastaa wa Bongo, awamu hii ni zamu ya Hamis Ramadhan ‘H.Baba’ ambaye kuvunjika kwa uhusiano wake na Flora Mvungi, kumbe inadaiwa amepinduliwa, Amani limeibumburua.
Habari zilizotua kwenye dawati juzikati kutoka kwa rafiki wa karibu na Flora, zinadai chanzo cha penzi hilo kuvunjika ni kutokana na msanii huyo kukolea kimahaba kwa kijana mmoja mtanashati anayejulikana kwa jina la Muddy P Didy.“Sikia bwana, msiumize vichwa nyenu bure, kuna jamaa anaitwa Muddy P Didy, ana duka la kuuza filamu Kariakoo (Dar), huyu alianza kutoka na Flora zamani, sasa demu amekolea, muda mwingi yuko naye ndiyo maana kaamua kuachana na H.Baba,” kilisema kikulacho hicho huku kikitoa picha za jamaa huyo.
Baada ya kuzinyaka ‘mbivu’ hizo, mwandishi wetu alimtafuta Muddy P Diddy kwa njia ya simu na kufanikiwa kumuweka hewani, mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo:
Amani: “Haloo, habari kaka…”
Muddy: “Salama, nani mwenzangu?”
Amani: ‘Mwandishi wa gazeti la Amani, kuna habari moja inakuhu…’ (simu ikakatwa).
Amani: (linapiga simu tena).
Muddy: ‘Ee, habari gani tena hiyo?’
Amani: “Unamfahamu msanii wa filamu, Flora Mvungi?”
Muddy: “Ndiyo, kwani vipi?”
Amani: “Kuna habari kuwa wewe ndiyo chanzo cha penzi lake na H.Baba kuvunjika.
Muddy: “Kwani yeye Flora amesemaje? Ninachojua mimi na Flora tuna uhusiano wa kazi, lakini kama ni kweli itajulikana baadaye, lakini kwa sasa hebu niache kwanza nina majukumu bwana.
Amani: “Hebu kuwa mkweli kaka, maana tuna picha zako hapa.”
Muddy: “Uhusiano uliopo ni huo.”
Baada ya kusikia utetezi wa jamaa huyo, paparazi wetu alimtwangia simu Flora ili kuujua ukweli, alipopatikana
“Watu wanasema sana lakini ukweli ni kwamba kwa sasa nimechoka na mambo ya mapenzi, huyo Muddy namjua kikazi jamani, mbona mnafuatafuata siri za watu nyiye, wanaosema waendelee na maneno yao.”
Gazeti hili lilipomtafuta H. Baba kwa njia ya simu, ilikuwa ikiita bila majibu na wakati mwingine kukatwa.

0 Comments