Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akizungumza na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa, katika mkutano uliofanyika siku ya jumatano na kuhudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu, Asha-Rose Migiro, Katika Katibu Mkuu alianisha Mpango Kazi wa miaka mitano pamoja na vipaumbele vitano. baadhi ya vipaumbele hivyo, ni pamoja na uwezeshaji wa wanawake ili waweze kushika nafasi za uongozi za kisiasa halikadhalika kuwawezesha kiuchumi pamoja na kushughulika masuala ya vijana.Kuzihamasisha nchi kupinga kwa nguvu zote ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Kusimamia maendeleo endelevu na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia, mabadiliko ya tabia nchi, kuimarisha utoaji wa huduma za dharura na misaada ya kibinadamu, kuzisaidia nchi ambazo zimetoka katika migogoro na kusimamia suala zima la upokonyaji wa silaha. Mara baada ya mazungumzo yake na Mabalozi,Ban Ki Moon alikutana na waandishi wa Habari ambapo pia alielezea vipaumbele hivyo na pia kutangaza mabadiliko makubwa ya safu ya uongozi katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa. Akielezea mabadiliko hayo, Ban Ki Moom aliwaambia waandishi kwamba, Naibu Katibu Mkuu Migiro pamoja na Msimamizi Mkuu wa Ofisi yake Bw. Vijay Nambier wamewasilisha kwake ombi la kuachia nafasi zao ili kumpisha kuunda safu mpya ya wasaidizi wake. Katika mabadiliko hayo wapo pia maafisa waandamizi kutoka Idara na Mifuko ya Umoja wa Mataifa, ambao nao pia wataachia nafasi zao. wengi wao ni wale ambao wamefanya kazi na Katibu Mkuu katika miaka mitano ya kwanza ya uongozi wake.
Na Mwandishi Maalum
New York
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon ametangaza kuwapo kwa mabadiliko makubwa katika safu ya uongozi ndani ya Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,mara baada ya kuainisha Mpango Kazi na Vipaumbele vya miaka mitano ya mwisho ya uongozi wake. Ban Ki Moon amethibitisha kwamba Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Asha- Rose Migiro atamaliza muda wake akiwamo pia Bw. Vijar Nambiar ambaye ni Mkuu wa Ofisi yake ( Chef de Cabinet).
“ Kama mlivyotangaziwa mwishoni mwa mwaka jana kuhusu mabadiliko yanayotarajiwa katika nafasi za watendaji waandamizi. Ningependa kuongezea na kuwajulisha kwamba, Naibu Katibu Mkuu, Bibi.Migiro na Bw. Vijar Nambiar wamewasilisha kwangu maombi yao ya kutaka kuachia nafasi zao , ili kuniruhusu kuunda timu mpya ya maafisa waandamizi nitakaofanya nao kazi katika awamu ya pili ya uongozi wangu” akasema Ban Ki Moon.
Na kuongeza “ Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Naibu Katibu Mkuu, Asha- Rozi Migiro, kwa uamuzi wake huo, na kwa kazi nzuri na ushirikiano mkubwa na usio na shaka wala doa alionipatia katika kipindi chote miaka mitano iliyopita akiwa msaidizi wangu wa karibu.
“ Amenipatia ushirikiano mzuri sana, alinishauri kwa busara na amejituma sana na kwa kuadilifu mkubwa katika kukabiliana na changamoto nyingi zilizoikabili Taasisi hii wakati wa awamu yangu ya kwanza ya uongozi” akasisitiza Ban Ki Moon.
Katibu Mkuu wa UM, akawaeleza waandishi wa habari kwamba, Naibu Katibu Mkuu, Migiro ataendelea kuwapo ofisini hadi mwezi wa sita mwaka huu ili kuratibu na kusimamia kipindi cha mpito pamoja na maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa wa Maendeleo Endelevu (RIO+20).
Kwa mujibu wa Ban Ki Moon, pamoja na Migiro kuwasilisha ombi lake wapo pia baadhi ya watendaji waandamizi ambao nao wameonyesha nia ya kuachia nafasi zao ili kupisha menejimenti mpya.
Miongozi mwa maafisa hao ni pamoja na kama ilivyoelezwa awali ni Msimamizi Mkuu wa Ofisi yake Bw. Vijay Nambiar ambaye katika muda muafaka atapewa kazi ya kuwa mshauri wa Katibu Mkuu kuhusu Mynmar.
Watendaji wengine watakaondoka na ambao wengi wao walikuwa katika awamu ya kwanza ya uongozi wa Ban Ki Moon ni kutoka Idara za Utawala, Maendeleo, Huduma za Mikutano, Habari, Ofisi ya Opokonyaji wa silaha, na Mshauri wa Masuala ya Afrika.
Wengine ni wasimamizi wa Idara za Uchumi za Afrika na Ulaya, waratibu wa mifuko ya maendeleo na Idadi ya watu UNDP na UNFPA. Aidha wamo pia wawakilishi maalum wa Katibu Mkuu wanaohusika na masuala ya watoto katika migogoro ya kivita, na uzuiaji wa mauaji ya kimbali, ambao wanatarajiwa kuachia nafasi zao kati kati ya mwaka huu.
Akaeleza pia kwamba mchakato wa kujaza nafasi Nane zitakazoachwa wazi katika ngazi za ukatibu mkuu msaidizi (Under-Secretary General) umekwisha anza .
Akasema ujazaji wa nafasi hizo ambao utakuwa wa uwazi utazingatia sana sifa na uwezo wa mtu, uwiano wa kikanda na jinsia
0 Comments