KAMATI ya Muda ya Jumuiya ya Madaktari wanaoendelea na mgomo nchi nzima imesema hawajafunga milango ya mazungumzo na ujumbe wowote kutoka kwa Waziri Mkuu.

Wameshangaa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kutowafuata walipo madaktari wote kama alivyofanya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, mwaka 2005 na badala yake juzi kuzungumza na waandishi wa habari.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Stephen Ulimboka alisema hayo jana katika kikao cha madaktari hao walichokihamishia katika ukumbi wa Starlight baada ya ukumbi wa Don Bosco kushindwa kuchukua madaktari wote waliojitokeza jana.

Juzi Pinda, alisema haoni sababu ya kukwama kwa mazungumzo kati ya Serikali na madaktari hao na kwamba yupo tayari kukutana na wawakilishi wao na kutuma salamu popote walipo na wakisikia ujumbe wake, wafike wamwone kabla hajaenda bungeni Dodoma, Jumamosi.
Awali walielezwa kuwa Jumanne, Pinda angefika kuonana nao, lakini iliishia kuonana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya, katika kikao walichokaa hadi saa tatu usiku bila mwafaka.




Kutokana na hatua hiyo, walimtaka Pinda afike na kuonana nao, kwani wao wapo tayari kumsikiliza pamoja na ujumbe wake, ili kufikia muafaka wa malalamiko yao na kuendelea kutoa huduma.

Wakati madaktari hao wakiendelea na kikao chao ambacho jana kilifurika zaidi, huduma katika hospitali za Serikali zimezidi kudorora na wagonjwa kurudishwa nyumbani huku wakitakiwa kurudi watakaposikia tangazo kwenye vyombo vya habari.

Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Kitengo cha Watoto hali ilizidi kuwa mbaya baada ya watoto wenye ugonjwa wa upungufu wa damu - selimundu, kutakiwa kurejea nyumbani na kurudi Alhamisi ijayo.

Pia watoto wenye matatizo ya moyo walitakiwa kurudi wiki ijayo jambo ambalo ni hatari, kutokana na kuwa watoto hao walitakiwa kusafiri wiki ijayo, kwenda India kwa matibabu.
Muhonewa Mfaume, mama wa Hamida mwenye umri wa miaka miwili na nusu, mwenye matatizo ya moyo na mkazi wa Kigoma aliyefikia Mwananyamala kwa ajili ya matibabu ya mtoto wake, alisema aliishakamilisha tararibu zote za Wizara ya Afya na alichobakiza ni kuonana na daktari ili ajaziwe fomu itakayomwezesha kwenda kuchukua viza kwa ajili ya kwenda India.

Alisema cha kushangaza ni kuwa jana alifika kumwona daktari, lakini akaambiwa arudi wiki ijayo, kutokana na maelezo kwamba madaktari wa kumwandikia hawapo.

“Acha nirudi nyumbani nikaendelee kumwomba Mungu tufike hiyo Ijumaa na Mungu ajalie wawe wamemaliza mgomo wao, kwani huyu mtoto kufika umri huu ni neema ya Mungu, hawezi kukakaa wala kusimama, hata kuongea anaongea kwa shida akizungumza sana anashindwa kupumua,“ alilalamika mama huyo.

Katika kitengo hicho, mmoja wa madaktari wanafunzi wa mwaka wa nne, alisema hali ni mbaya, kwani huduma zote za wagonjwa wa nje zimesitishwa, labda kwa wenye hali mbaya sana na waliolazwa.

Alisema wanaofanya kazi sasa ni wao, walio katika mafunzo na wahadhiri wanaofundisha Chuo Kikuu cha Muhimbili, ambao ni wataalamu wa watoto, lakini hutoa huduma mara chache sana.

Katika Kitengo cha Wagonjwa wa Nje, ilionekana misururu mirefu ya wagonjwa wakisubiri madaktari, huku ikionekana kuwapo madaktari katika vyumba lakini wakidaiwa kuwa wanafunzi.

“Mimi ni daktari wa Kitengo hiki cha Wagonjwa wa Nje na wote tupo kwenye mgomo, ninachoshangaa hao wanaotoa huduma wametoka wapi, kwani siwatambui, hebu jaribuni kuwauliza,” alisema mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo aliyekataa kutaja jina.
Baadaye ilionekana wagonjwa hao wakirejeshewa fedha walizotoa kwa ajili ya vipimo na kumwona daktari.

<><> <><>
Ramadhani Makuka wa Kimara anayesumbuliwa na tumbo, aliandikiwa na daktari afike jana lakini alipofika aliandikiwa arudi Machi 22.

Hali mbaya zaidi, ilionekana katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) ambapo wagonjwa waliondolewa na kutakiwa kurejea mara watakaposikia tangazo katika vyombo vya habari.

Mgonjwa wa mgongo, Rukia Hamis, mkazi wa Ununio alisema amesikitishwa kwa baadhi ya maofisa kuwasumbua na kutumia gharama kufika hospitali baada ya kuelezwa kuwa hakuna mgomo lakini kumbe upo.

Bryceson Sauli, aliyepata ajali ya mguu, alisema ifike mahali wagonjwa nao waandamane kuhakikisha Serikali inawasikiliza madaktari, ili waweze kupata haki zao za matibabu.

Huduma katika Hospitali za Amana na Temeke pia zilikuwa za kusuasua, huku wakionekana idadi kubwa ya wagonjwa wa nje wakirejeshwa nyumbani.

Dk. Ayub Kibao, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Amana alisema wameamua kusitisha huduma za wagonjwa wa nje, baada ya madaktari wanafunzi kuendesha mgomo.
Mgomo wa madaktari ulianza rasmi Jumanne na umeendelea kadri siku zinavyosonga mbele.