SERIKALI imekamilisha ujenzi wa mahema yenye uwezo wa kuhifadhi kaya 100 za wananchi waliokumbwa na maafa ya mafuriko Desemba mwaka jana katika Jiji la Dar es Salaam.
Makazi hayo yako katika eneo la Mabwepande, wilayani Kinondoni nje kidogo ya Jiji na sasa waathirika hao, wengi wao wakiwa katika kambi za dharura za Mbweni na Ubungo Maziwa, watahamia katika eneo hilo kupisha shule kufunguliwa leo.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana akizungumza na gazeti hili Mabwepande jana, alisema wakazi hao watahamia katika eneo hilo kwa awamu.
Kwa mujibu wa Rugimbana, kati ya kaya 100 hadi 150 zinatarajiwa kukabidhiwa maeneo yao ya ukubwa wa mita 16 kwa 26 wakati wowote wiki hii.
Pia Serikali inakamilisha mchakato wa kuwahamishia katika shule za karibu na eneo hilo, wanafunzi 1,200 waliobainika katika kaya zilizoathirika pamoja na kuwapa vifaa vya shule
zikiwemo sare, madaftari na kuweka vituo vya daladala ili kuwawezesha kuendelea na masomo mapema iwezekanavyo.Rugimbana alisema tayari eneo la kaya 100 litakabidhiwa kwa Serikali leo jioni na kaya nyingine 50 zitakamilika kesho ili kuwezesha waathirika kuhamia kwa awamu.
Hata hivyo Rugimbana alisema idadi kamili ya waathirika watakaopewa maeneo hayo yaliyotolewa bure na Serikali bado inaendelea kufanyika kazi na akaahidi idadi itajulikana leo wakati taarifa rasmi ikitolewa kwa Mkuu wa Mkoa.
“Tunaweza kupaita hapa ni kambi kwa kuwa tumejenga mahema kwa dharura kwa ajili ya waliokuwa kwenye makambi…kambi hii itaendelea kwa angalau miezi mitatu kwa kutoa ulinzi, maji, chakula kwa siku chache ili wazoee mazingira kisha watajitegemea baada ya hapo,” alisema Rugimbana.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema eneo hilo lililokuwa mali ya Serikali, lina ukubwa wa ekari 1,500 na tayari waliokuwa wanapaswa kulipwa fidia awali walishalipwa na wachache waliobakia mchakato unakamilika.
Aliwaonya wavamizi katika eneo hilo waondoke kwa kuwa eneo lote ni la mradi huo na baadaye wataruhusiwa watu wengine kununua.
Kuhusu tathmini upya, Rugimbana alisema, Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu
Kitengo cha Maafa wanasimamia kazi hiyo kuhakikisha walengwa wanapata viwanja hivyo kama Rais Jakaya Kikwete alivyoagiza.
Alisema uongozi wa Mkoa utafanya tathmini mpya itakayohusisha waathirika na nyumba zao
kupigwa picha sambamba na aina za nyumba ili kuepusha utapeli. Aliwashukuru watu binafsi na kampuni mbalimbali kwa msaada wao wa vifaa vya ujenzi, vyakula, nguo na maji kwa waathirika.
Rugimbana alisema misaada ya ujenzi kama saruji itatumika kujenga shule, zahanati na kituo cha Polisi na miundombinu mingine ya jamii na haitagawiwa kwa mtu binafsi.
Naye Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Ismail Mafita ambaye ni Meneja Mradi wa Kuhamisha Waathirika wa Mafuriko, alisema tayari viwanja 268 vya mita 16 kwa 26 vimekamilika.
Alisema kinachoendelea ni ujenzi wa mahema unaofanywa kwa ushirikiano wa Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Gazeti hili likiwa eneo la tukio jana, lilishuhudia wanajeshi na maofisa wa Msalaba Mwekundu
wakiendelea na ujenzi wa mahema, mabafu, vyoo vya dharura na kuweka matangi ya maji ya ujazo wa kati ya lita 1,000 na 2,000 .
Kila hema limejengwa katika pembe ya eneo husika na kutizama barabara ya mtaa, ili kumuwezesha muhusika kufanya ujenzi wa makazi ya kudumu baadaye.
Pia barabara kubwa ya upana wa meta 30 ilikuwa ikiendelea kujengwa mbali na barabara za mitaa ndani ya kambi hiyo na kulikuwa na usimamizi uliokuwa ukifanywa na maofisa wa Serikali walioweka kambi eneo hilo kuanzia Januari tatu mwaka huu.
“Barabara kuu licha ya upana wa meta 30 ina urefu wa kilometa 30, kazi ya kuchonga barabara inafanywa na mitambo ya kampuni mbili; Delmonte T (Ltd) wanaotengeneza kilometa 16.3 na Namis Corporate Ltd wenye kilometa 13.7; tunao wanajeshi 70 wanashiriki kwenye ujenzi kwa hiyo mambo ni mazuri,” alisema Mafita.
Alisema maeneo hayo yametengwa ili kuwezesha ujenzi wa dharura na kwamba eneo hilo la kwanza, lina ukubwa wa heka 340.
Waathirika waridhika Baadhi ya waathirika waliokuwa eneo hilo jana, walionesha kustaajabu
uzuri wa eneo hilo na kueleza wazi kuwa wameridhika na hatua hiyo ya Serikali na wakataka watakaogoma kuhamia huko, Serikali isihusike nao tena na wadanganyifu wadhibitiwe.
“Kwa kweli tumeridhika, eneo ni zuri, tunaomba walengwa tu wapewe maana wadanganyifu hawakosekani, tunaomba pia Serikali itusaidie kuhamisha vifaa vilivyosalia kama mabati na matofali hadi eneo hilo,” alisema Anna John, muathirika mwenye nyumba namba B114 eneo la
Jangwani.
John aliungwa mkono na muathirika mwingine Dotto Kaji mwenye nyumba namba C 32 katika
eneo la Mchikichini.
Mafuriko hayo yalisababisha watu zaidi ya 40 kupoteza maisha huku wengine zaidi ya 5,000 wakikosa makazi baada ya nyumba zao kufunikwa na maji ambapo Serikali ilitangaza
uamuzi wa kuhamishiwa waathirika wenye nyumba katika maeneo hayo ya mabondeni.
0 Comments