MWANAFUNZI wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Edmubdrise, inayomilikiwa
na Kanisa Katoliki Jimbo la Arusha, John Justine (17) amejiua kwa kujipiga risasi kifuani.

Justine amejiua kwa kutumia bunduki ya baba yake mzazi aina ya shotgun, baada ya kutuhumiwa na baba yake Justine Kaiza kuwa amemuibia fedha taslimu dola za Marekani 1,500.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye amethibitisha kutokea habari za
kujiua kwa John na kusema kuwa alifanya hivyo juzi usiku majira ya saa 1:30 katika eneo la Makao mapya Kata ya Levolosi jijini Arusha.

Kamanda Andengenye alisema mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Betty Mushi alidai kuwa
yeye alikuwa katika sherehe na aliporudi nyumbani kwake, alikuta lango kuu limefungwa
akagonga ili afunguliwe lakini hakufunguliwa.

Alisema mara baada ya kuona kimya hicho, alimuomba mtoto wa jirani amfungulie lango hilo na lilipofunguliwa alimkuta mwanawe amelala chini akihema kwa tabu huku akivuja damu
nyingi kifuani. Kamanda Andengenye alisema mama huyo aliendelea kueleza kuwa baada ya kumkuta mtoto
wake katika hali hiyo aliita majirani zake ambapo walimchukua mtoto huyo hadi katika Hospitali ya Athna Asher Charitable maarufu kwa Dk. Mohamed na baadae alihamishiwa hospitali ya Mount Meru.

Alisema akiwa katika hospitali ya Mount Meru akiendelea kupatiwa matibabu, mwanawe huyo alifariki dunia kutokana na jeraha hilo la risasi pamoja na kuvuja damu nyingi kwa kipindi kirefu.

Kamanda Andengenye alisema mara baada ya taarifa hizo kufika polisi, askari walikwenda eneo la tukio na kukuta bunduki hiyo chini na ujumbe wa maneno katika karatasi unaosadikiwa
kuandikwa na John usemao; ”nasikitika kulaumiwa na wazazi wangu na pia ninawapenda sana.”

Aidha katika ukaguzi wa polisi walikuta michirizi ya damu kutoka ndani ya chumba alichokuwa
akilala John hadi nje ya nyumba hiyo mahali alipoangukia.

Polisi wanamshikilia baba wa marehemu kwa mahojiano kuhusu kifo hicho na umiliki wa
silaha hiyo kwa kuwa inadaiwa na ndugu wa familia kuwa John aliuawa na baba huyo kutokana na upotevu huo wa pesa pamoja na madai kuwa bunduki hiyo haimilikiwi kihalali.