ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo, amesema yeye si mfanyabiashara wa dawa za kulevya ila anatajwa kwa nia ya kunyamazishwa asizungumze ukweli.
Kardinali Pengo akizungumza na vijana katika ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Kawe jana alisema hajapata kuona wala kujua dawa za kulevya, lakini anajua anatajwa hivyo na wanaotaka anyamaze.
“Mimi mwenyewe nimewekwa katika orodha ya dawa za kulevya, naona kwenye vyombo vya habari, dawa zenyewe wala zisijui, lakini naendelea kuzungumza kwa sababu najua yanafanywa na wanaotaka kuninyamazisha … sitanyamaza ng’o,” alisema Pengo.
Alikuwa akiwaeleza vijana kuhusu utandawazi na kuwataka waache kuyumbishwa na
kuamini kila wanachoona kimeandikwa kwenye mtandao.
Alisema mambo mengi ya ajabu yamekuwa yakiandikwa na kusemwa, lengo ikiwa ni
kunyamazisha maaskofu na mapadri wasiendelee kufundisha ukweli, ili watu wachache wafaidike.
“Ni uzushi unaofanywa na watu kuharibu na kuchimbachimba Kanisa tusiseme ukweli,
wachache waendelee kufaidika, naomba vijana msisombwe na hali hii, kwani watu hawa hawana woga ili mradi lengo lao la kuharibu Kanisa lifanikiwe …
vijana mna uhai
ndani yenu na mna uwezo kama maaskari wa kupambana na waovu wa Kanisa,” alisema.
“Silaha ya vijana ni maisha yanayojua mnaamini kitu gani, msikubali kuyumbishwa na watu wanaotoa mambo vichwani mwao. Kama mnasikia natajwa, njooni mniulize, Baba mbona nimesikia habari fulani, badala ya kuyabeba na kushabikia…imani yenu si ya kutetereka, endeleeni kuwa imara watetereke wanaotaka tutetereke,” alisema.
Alisema vijana pia wamekuwa wakitumika kama vyombo katika biashara ya kulevya huku watu wachache wakitajirika na kwamba baadhi yao wanaokemea au kuzungumzia, wanapuuzwa au kuambiwa ndio wafanyabiashara wa dawa hizo, jambo ambalo nyuma yake halina ukweli wowote.
Kardinali Pengo alisema lengo ni kutaka kuwanyamazisha watu wanaosema ukweli ili wachache waendelee kutajirika na biashara hiyo kwa kuwatia hasara vijana.
Naye Mhashamu Askofu Salutaris Libena, ambaye aliongoza Ibada Takatifu, alisema vijana
wamekutana ili kumshukuru Mungu na kumwomba neema .
Libena ambaye pia ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, aliwataka vijana kuingia mwaka mpya kwa kumjua na kumtukuza Mungu. Mbali na vijana kushiriki ibada hiyo lakini pia zilikuwapo burudani mbalimbali za kwaya na ngoma, sambamba na vijana kupima kwa hiari damu kwa ajili ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama.
Kila mwisho wa mwaka vijana kutoka makanisa mbalimbali ya Kanisa Katoliki hukutana
kwa lengo la kumtukuza Mungu na kumshukuru kwa kumaliza mwaka.
0 Comments